Ujerumani yaijaribu EU kwa kuongeza udhibiti mipakani
10 Septemba 2024Mwezi uliopita, shambulio hatari la kisu mjini Soligen liliwaua watu watatu. Mshambuliaji alikuwa mtafuta hifadhi kutoka Syria ambaye alidai kuongozwa na kundi la Islamic State. Mwezi Juni, shambulio jingine la kisu lililofanywa na mhamiaji kutoka Afghanistan liliua afisa mmoja wa polisi na kuwajeruhi watu wengine wanne.
Lakini majirani wengi wa Ujerumani ni wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), kundi la nchi 27 lililojengwa kwa misingi ya biashara huru na usafiri. Na Ujerumani — injini ya kiuchumi ya EU iliyoko katikati ya Ulaya — inashiriki mipaka mingi na nchi nyingine kuliko nchi nyingine yoyote mwanachama wa EU.
Kufungwa kwa mipaka kunatarajiwa kuanza wiki ijayo na kudumu kwa miezi sita — hatua ambayo tayari inatishia kuvunja umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Poland alilaani vikali hatua hizo kama "zisizokubalika" na Austria ikasema haitapokea wahamiaji waliokataliwa na Ujerumani. Haya ni baadhi ya masuala yanayozungumzwa:
Raia wa Ulaya wanasafirije sasa?
Kanda ya Umoja wa Ulaya ina eneo la usafiri bila viza linalojulikana kama Schengen ambalo linawaruhusu raia wa nchi nyingi za EU kusafiri kirahisi kuvuka mipaka kwa ajili ya kazi na starehe. Iceland, Liechtenstein, Norway, na Uswisi pia ni wanachama wa Schengen ingawa si wanachama wa EU.
Soma pia: Ujerumani kuongeza kasi ya kuwarudisha wahamiaji makwao
Kwa mujibu wa EU, nchi wanachama zinaruhusiwa kuanzisha upya udhibiti wa muda kwenye mipaka ya ndani ya EU endapo kuna tishio kubwa, kama vile usalama wa ndani. Lakini pia inasema udhibiti wa mipaka unapaswa kuwa hatua ya mwisho katika hali za kipekee na lazima iwe na mipaka ya muda.
Mara nyingi vikwazo hivyo huwekwa wakati wa matukio makubwa ya michezo, ikiwemo Michezo ya Olimpiki iliyopita mjini Paris, na mashindano ya soka ya Ulaya msimu huu wa joto.
Ujerumani inafanya nini sasa?
Nchi tisa zinapakana na Ujerumani — idadi kubwa zaidi katika EU — na zote ni sehemu ya Schengen. Ujerumani tayari iliweka udhibiti mwaka jana katika mipaka yake na Poland, Jamhuri ya Czech, Austria, na Uswisi.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani Jumatatu iliagiza kuendeleza ukaguzi kwenye mipaka hiyo, pamoja na udhibiti kwenye mipaka ya Ufaransa, Luxembourg, Uholanzi, Ubelgiji, na Denmark.
Waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Faeser alisema lengo ni kupunguza uhamiaji usio wa kawaida na kuilinda nchi dhidi ya "hatari kali zinazosababishwa na ugaidi wa Kiislamu na uhalifu mkubwa."
Kufufuka kwa upinzani dhidi ya uhamiaji
Serikali na Wajerumani wengi waliwakaribisha wakimbizi waliokuwa wakikimbia migogoro nchini Syria na kwingineko kuanzia 2015-16, wakati ambapo watu zaidi ya milioni moja waliomba hifadhi nchini humo. Lakini kadri uhamiaji mkubwa ulivyoendelea Ulaya kwa karibu muongo mmoja sasa, upinzani umekuwa ukichochea kuongezeka kwa vyama vya mrengo wa kulia.
Soma pia: Chama cha CDU chataka hatua kali dhidi ya uhamiaji Ujerumani
Watu wanahisi kuwa huduma za kijamii zimezidiwa, na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na watafuta hifadhi yamesababisha hofu ya kiusalama. Hali hii imepelekea ongezeko la uungwaji mkono kwa sera kali za uhamiaji — na kwa baadhi ya matukio, kuviimarisha vyama vya mrengo wa kulia vinavyotetea vikwazo hivyo.
Serikali ya mseto isiyopendwa ya Kansela Olaf Scholz sasa inajaribu kudhibiti uhamiaji usio wa kawaida baada ya mrengo wa kulia kufanya vizuri kwenye chaguzi mbili za majimbo mashariki mwa Ujerumani. Chaguzi nyingine inatarajiwa kufanyika Septemba 22 huko Brandenburg, jimbo linalozunguka Berlin.
Wasiwasi wa kiuchumi
Kama taifa lenye uchumi mkubwa zaidi katika EU, Ujerumani ni mshirika muhimu wa kibiashara kwa majirani zake. Tangazo la wizara ya mambo ya ndani tayari limezua wasiwasi wa kiuchumi kwa kundi la uraghibishi la wasafirishaji nchini Uholanzi, Chama cha Usafirishaji cha Uholanzi. Shirika hilo limesema uamuzi huo unadhoofisha kanuni ya Schengen ya biashara huru na linaogopa uharibifu mkubwa wa kiuchumi.
Huko nyumbani, chama cha usafirishaji cha DSLV cha Ujerumani kiliomba njia ya kuchagua ambayo ingeyaondolea malori yanayosafirisha bidhaa kuvuka mipaka — kama ilivyofanyika wakati wa mashindano ya soka ya Ulaya. Ukaguzi wa msimu huu wa joto uliweza kuepuka kuvuruga uchumi kwa sababu maafisa walilenga watu binafsi na sio malori, shirika hilo limesema.
Dirk Jandura, rais wa Shirikisho la Ujerumani la Biashara ya Jumla, Biashara ya Kigeni na Huduma, alisema katika taarifa kwa Associated Press kuwa vikwazo vya uhuru wa kusafiri "huashiria ucheleweshaji na hivyo ongezeko la gharama kwa uchumi, hasa kwa biashara ya jumla na biashara ya nje."
"Vinavuruga usafirishaji na hivyo kuvuruga minyororo ya ugavi," aliandika. "Hata hivyo, ikiwa sera ya uhamiaji inahitaji hatua za kudhibiti, basi hili linaeleweka. Kwetu, ni muhimu kutekeleza hatua hizo kwa uwiano sahihi."
Athari za kisiasa
Serikali ya kihafidhina inayotawala nchini Austria — ambayo inakabiliwa na ushindani mkali dhidi ya chama cha mrengo wa kulia kwenye uchaguzi utakaofanyika baadaye mwezi huu — imesema haitapokea wakimbizi wanaorejeshwa kutoka Ujerumani jirani.
Waziri wa Mambo ya Ndani Gerhard Karner aliwaambia waandishi wa habari kuwa Ujerumani ina haki ya kuwarudisha watu ikiwa nchi nyingine ya EU inawajibika kwa maombi yao ya hifadhi. Lakini hilo litahitaji utaratibu rasmi na ridhaa ya nchi mwanachama inayohusika.
Soma pia: Kushamiri kwa itikali kali za kulia huenda kukazuwia uhamiaji wafanyakazi wenye ujuzi
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk aliita mpango wa Ujerumani "usiokubalika" na akaitisha mashauriano ya dharura kwa nchi zote zilizoathiriwa. Poland imekuwa ikikabiliana na mgogoro wa uhamiaji kwenye mpaka wake na Belarus tangu 2021. Warsaw inaituhumu Belarus na Urusi kwa kuvutia wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati na Afrika kuja huko ili kudhoofisha Magharibi.
Lakini huko Uholanzi, ambako chama cha kupinga uhamiaji cha Party for Freedom kilishinda uchaguzi mwaka jana, waziri wa hifadhi na uhamiaji aliahidi kuongeza udhibiti wa mipaka ya Uholanzi pia.
Slovenia, Austria na Italia pia zimesogeza mbele udhibiti wa mipaka kwa muda katika baadhi ya maeneo au mipaka yote.