Ujerumani kuongeza kasi ya kuwarudisha wahamiaji makwao
26 Agosti 2024Kansela Scholz aliweka shada la maua kwenye eneo la shambulizi katika mji huo wa Solingen. Shambulio hilo lilitokea Ijumaa jioni wakati wa tamasha la kusherehekea maadhimisho ya miaka 650 ya jiji hilo.
Wanaume wawili, wenye umri wa miaka 67 na 56, na mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 56 waliuawa. Watu wanane walijeruhiwa, na wanne kati yao wamo katika hali mahututi kulingana na msemaji wa polisi wa Solingen.
Katika hotuba yake, kansela wa Ujerumani alionyesha hasira yake dhidi ya watu wenye misimamo mikali. Scholz ameahidi kuimarisha sheria za silaha na kukabiliana na wahamiaji haramu. Amesema shambulio hilo baya la kisu la wiki iliyopita ni kitendo cha kigaidi dhidi ya wote.
Soma Pia: Mshukiwa wa shambulio la Solingen kufikishwa mahakani Karlsruhe
Shambulio hilo limezusha mjadala kuhusu uhamiaji wakati ambapo uchaguzi unakaribia katika majimbo mawili ya Ujerumani Mashariki ya Saxony na Thuringia.
Mashambulizi katika mji wa Solingen yameongeza ukosoaji kwa serikali ya kansela Olaf Scholz katika kushughulikia maswala ya uhamiaji.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,cha AfD, kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani na kinachopinga wahamiaji kimezishutumu serikali ya sasa na iliyotangulia kwa kusababisha machafuko kutokana na kuruhusu wahamiaji wengi kuingia nchini humo.
Kiongozi mwenza wa chama hicho cha AfD, Alice Weidel, ametoa wito wa kuacha kuwadekeza wahamiaji, na pia kufuta muda wa miaka mitano kwa wahamiaji kupata uraia wa Ujerumani.
Wakati huo huo, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CDU Friedrich Merz, ameitaka serikali kuacha kuwapokea wakimbizi kutoka Syria na Afghanistan.
Msemaji wa kansela wa Ujerumani Steffen Hebestreit amesema katika mkutano wa waandishi wa habari kwamba kusimamishwa kabisa maombi ya hifadhi kutoka kwa raia wa nchi hizo hakuambatani na katiba ya Ujerumani.
Soma Pia: Mauaji ya Solingen na ustawi wa kina mama wadogo Ujerumani
Kwa upande mwingine, serikali ya kansela Scholz tayari ilikuwa chini ya shinikizo la kuanzisha tena zoezi la kuwarudisha nyumbani raia wanaotoka Afghanistan na Syria, baada ya kusimama kwa miaka kadhaa.
Wajumbe wa muungano unaotawala walitoa wito kama huo wa kuchukuliwa hatua kali za kuwafukuza wakimbizi baada ya raia wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 25 alipomdunga kisu afisa mmoja wa polisi katika mji wa Mannheim mnamo mwezi Mei.
Vyombo vya usalama vya Ujerumani vimekuwa katika hali ya tahadhari tangu vita vya Gaza vilipoanza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kuishambulia Israel.
Vyanzo: DPA/AFP