Scholz aunga mkono kufukuzwa wahalifu wa Syria, Afghanistan
6 Juni 2024Akihutubia bunge la Ujerumani, Bundestag, Alhamisi, Scholz amesema uhalifu na vitisho vya kigaidi havina nafasi nchini Ujerumani. "Lakini pia niweke wazi. Ninakasirishwa wakati mtu ambaye ametafuta hifadhi hapa anafanya uhalifu mkubwa zaidi. Wahalifu kama hao wanapaswa kufukuzwa, hata kama wanatoka Syria na Afghanistan."
Soma pia: Polisi wa Ujerumani wanamshikilia mshukiwa wa tano katika njama ya kanisa kuu la Cologne
Hata hivyo, Scholz hakutoa ufafanuzi kuhusu jinsi hatua hiyo itakavyotekelezwa. Lakini alisema Wizara ya Mambo ya Ndani ilikuwa ikifanyia kazi utekelezaji wake rasmi, na tayari wanaendesha mazungumzo na majirani wa Afghanistan.
Kauli hii ya Kansela Scholz inajiri siku chache baada ya afisa mmoja wa polisi kuuwawa kufuatia shambulio la kisu na raia wa Afghanistan kwenye mji wa kusini magharibi wa Mannheim.