Nakuru yapandishwa hadhi na kuwa jiji
4 Juni 2021Gavana wa kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui anasema mji huu uliojulikana kama kiunganishi cha watu wa jamii tofauti umepata kitambulisho kipya kwa kuwa jiji la nne nchini Kenya.
Safari hiyo iliyochukuwa zaidi ya miaka mitatu imekamilika baada ya bunge la seneti kuupitisha mswada ulioidhinisha mji wa Nakuru kufanywa jiji.
Kati ya vigezo vilivyochangia hatua hii ni namna serikali ya kaunti ya Nakuru ilivyoimarisha sekta za utalii, viwanda, miundo mbinu pamoja na afya.
Soma pia: Wahudumu wa afya Nakuru walalamikia mazingira duni ya kazi
"Tumekuwa na safari ndefu na isiyo rahisi hadi kufikia bunge la seneti. Nakuru ya sasa itakuwa tofauti na ya miaka mitano ijayo," alisema gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui.
"Kutakuwa na fursa zaidi, maeneo ya makongamano yataimarika, kutakuwa na wageni zaidi, chakula kitauza zaidi, hitaji la huduma za uchukuzi na burudani litaongezeka.”
Je, Nakuru iko tayari kwa changamoto ya kuwa jiji?
Kumekuwa na maswali yanayoibuka kuhusu utayari wa mji wa Nakuru kwa hadhi iliyopewa. Baadhi ya wadau wanahoji kwamba mji huu hauna ardhi ya kutosha kwa ajili ya upanuzi, hauna mfumo thabiti wa usimamizi wa taka na majitaka, na wanahofia utozaji wa ada za juu kwa biashara zao, kati ya mengineyo.
Lakini akiangazia changamoto zilizopo, Gavana wa NakuruLee Kinyanjui amesema wameweka mikakati na mipangilio ya kuanisha sera na masharti yatakayomzingatia mwananchi.
Soma pia: Siasa za Kenya zachukua mkondo wa 2007
"Ni kweli watu wengi hawajui inamaanisha nini kuwa kwenye jiji, kwa sababu hawajawahi kuwa hapo. Tutawashirikisha kwa karibu ndiposa matarajio yao yaweze kulingana na maono yetu," alisema gavana Lee.
Hatua inayosubiriwa ni kwa Rais Uhuru Kenyatta kuliratibisha tangazo hili kwenye gazeti rasmi la serikali. Na kama anavyoeleza Gavana Lee, watamkaribisha Rais kwenye sherehe rasmi ya kuwakabidhi wananchi hati yenyewe.