Siasa za Kenya zachukua mkondo wa 2007
9 Septemba 2020Mvutano wa kisiasa unazidi kuwa mkubwa nchini Kenya baina ya wafuasi wa Naibu Rais William Ruto na wale wanaoonekana kuunga mkono mshikamano uliopo baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila odinga, na sasa viongozi wa Bonde la Ufa wanahofia matamshi ya hivi karibuni ya wabunge wa eneo hilo yanaibua taharuki za uwezekano wa kurejewa kwa ghasia zilizoshuhudiwa mwaka 2007 baada ya uchaguzi mkuu.
Idara za usalama, vyama vya kisiasa na mashirika mengine ya uongozi yamechukua hatua za dharura kuhakikisha amani inadumishwa, ila wafuasi wa Naibu Rais William Ruto wanashikilia kuwa anaandamwa bila sababu.
Soma pia: Raila akemea siasa za matusi Kenya
Dhoruba la kisiasa lililosababishwa na mbunge wa Emurua Dikir Johana Ngeno na mwenzake wa Eldoret Oscar Sudi ambao ni washirika wa Naibu Rais William Ruto walipomtusi Rais Uhuru Kenyatta na familia yake jumapili iliyopita, limeibua hali ya wasiwasi, hasa baina ya wakaazi wa eneo la Bonde la Ufa, ambapo viongozi wanauona mwelekeo huu kama tishio kwa juhudi za amani zilizochukuliwa. "Tunakashifu kwa njia kubwa sana.
Wacha huyu mbunge anaitwa Ngeno na yule mwingine anaitwa Sudi watafute wazee waongee waseme pole kwa Kenya nzima. Hiyo lazima wafanye,” alieleza Daktari Peter Mbae, mwakilishi katika bunge la kaunti ya Nakuru.
Siasa za Kenya zinahofiwa kufuata mkondo wa mwaka 2007 ambapo maelfu ya watu walipoteza maisha na wengine kupoteza mali na makaazi kutokana na ghasia zilizosababishwa na chuki baina ya makabila makubwa hapa nchini. Mbae anaendelea kwa kuonya kuwa, "kuna kitu kingine hata mtoto mdogo hawezi kuongea.
Lakini unaongea wewe kwa sababu unajua hata ukishikwa utakuwa na umaarufu. Eldoret ni mahali kila mtu anaishi. Kila mtu anakaa hapo. Kwa hivyo sisi tunasema tunataka adabu kwa siasa.”
Soma pia: Kenyatta na makamu wake Ruto waendelea kutofautiana
KANU yamvua uanchama mbunge Ngeno
Siku mbili baada ya matamshi ya wabunge hao, chama cha KANU kimetangaza kuwa kimeubatilisha uteuzi wa Johana Ngeno ambaye alichaguliwa kama mwakilishi wa bunge la kitaifa kupitia tiketi ya chama hicho. Na sasa KANU inataka kiti hicho kutangazwa wazi na uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Emurua Dikiri kufanyika.
Hata hivyo, wafuasi wa Naibu Rais Rutto wanakosoa jinsi wabunge walioko kwenye mrengo wake wanavyoshurutishwa na kunyimwa haki ya kujielezea wazi. Kimani Nginjiri mbunge wa Bahati anasema, "kama kuna mjumbe aliongea namna hiyo, sio Ruto aliongea. Murathe akiongea sio Kenyatta ameongea. Ruto akitaka kuongea atafanya nini, ataongea.”
Inspekta mkuu wa polisi Hilary Mutyambai amesema idara ya usalama iko macho kuchunguza matamshi pamoja na taarifa kwenye mitandao ya kijamii wakiwalenga wanasiasa wanaolaumiwa kwa kuchochea chuki baina ya Wakenya.
Soma pia:Ruto afungua ofisi sanjari ya chama cha Jubilee
"Tufahamu kwamba yeyote anayetishia au kuchochea vurugu ya kikabila, kidini au kisiasa atakabiliwa kwa mujibu wa sheria. Tumetambua kuwa kuna uchochezo mkubwa pia kwenye mitandao ya kijamii ambapo wanasiasa wanaazimia kuwafikia watumiaji wengi kwa kueneza porojo zao," alieleza Mutyambai.
Johana Ngeno ambaye alishtakiwa kwenye mahakama ya Nakuru yuko korokoroni kwa muda wa siku mbili akisubiri mashtaka dhidi yake. Afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma imeeleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa matamshi ya Mbunge huyo yalilenga kuchochea chuki za kikabila baina ya jamii tofauti zinazoishi eneo la Transmara.