Nagelsmann atumai Rudiger atacheza dhidi ya Denmark
29 Juni 2024Ujerumani itakabana koo na Denmark mjini Dortmund katika mechi ya usiku ikiwa na matumaini kuwa beki wa kati Antonio Rudiger atajumuishwa kikosini. Beki huyo mwenye umri wa miaka 31 alirejea mazoezini Ijumaa kufuatia jeraha la paja alilopata katika mechi waliyotoka sare ya 1 - 1 na Uswisi wakati Ujerumani ilimaliza kama kinara wa Kundi A.
Soma pia: Euro 2024: Timu 16 zajipanga katika hatua ya mchujo
Kocha wa Ujerumani Julian Nagelsmann amesema madaktari wamefanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa yuko sawa kurudi uwanjani. Rudiger huenda akashirikiana katika safu ya ulinzi na Nico Schlotterbeck, ambaye atachukua nafasi ya Jonathan Tah anayetumikia adhabu ya kadi za njano. Katika ushambuliaji, Nagelsmann alikataa kufichua ni nani atakayeanza kati ya Kai Havertz na Niclas Füllkrug.
Katika mechi ya mapema jioni, Uswisi itashuka dimbani dhidi ya mabingwa watetezi Italia. Kocha wa Uswisi Murat Yakin amesema anatumai kusababisha mshangao dhidi ya Wataliano mjini Berlin.