Euro 2024: Timu 16 zajipanga katika hatua ya mchujo
27 Juni 2024Katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, timu zote nne za Kundi E zilimaliza na pointi nne kila mmoja baada ya Ubelgiji na Ukraine kutoka sare ya 0 – 0 mjini Stuttgart na Romania na Slovakia kutoka sare ya 1 – 1 mjini Frankfurt.
Ubelgiji kwa kipindi kirefu haikuridhisha kwa mara nyingine na ililazimika kuwa makini kwa sababu ushindi kwa Ukraine ungewafurusha mashindanoni na walizomewa na mashabiki wao uwanjani baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa.
Matokeo hayo sasa yana maana kuwa Ubelgiji yake Kevin De Bryune itakabiliwa na kibarua kikali na Ufaransa yake Kylian Mbappe Jumatatu jioni. Wapinzani wa Slovakia watakuwa ni England Jumapili jioni.
Kulikuwa na uvumi kuwa Romania na Slovakia zingecheza tu kuanzia mwanzo zikitafuta matokeo ya sare kwa sababu yangeziingiza katika hatua inayofuata, bila kujali matokeo ya mechi ya Ubelgiji na Ukraine.
Lakini pande zote zilikanusha hilo, na Ondrej Duda akaifungia Slovakia bao la kichwa dakika ya 24. Razvan Marin akasawazisha kupitia penalti dakika 13 baadae.
Romania wanaongoza kundi na watacheza katika hatua ya mchujo kwa mara ya kwanza tangu 2000 dhidi ya Uholanzi Jumanne wiki ijayo.
Georgia wawaduwaza Wareno
Katika Kundi F, Georgia iliiduwaza Ureno na kutinga hatua ya mtoano, kwa mara yao ya kwanza kabisa katika mashindano makubwa- baada ya kuwafunga mabingwa hao wa zamani wa Ulaya – 2 – 0. Ureno ambao walikuwa tayari wamefuzu, walifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza. Khvicha Kvaratskhelia na penalty ya Georges Mikautadze ndiyo yaliwapa Georgia tiketi.
Ushindi huo wa kushangaza wa Georgia unawapa zawadi ya kukutana na Uhispania Jumapili usiku na una maana walifuzu kama moja ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi, Pamoja na Slovenia, Uholanzi na Slovakia.
Uturuki pia ilijiunga nao baada ya kuwatimua Waczech kwa kuwafunga 2 – 1 huku Hungary hatimaye wakikubali hatima yao.
Waczech, ambao walifika robo fainali katika mashindano yaliyopita ya Ulaya, walihitaji ushindi ili wawe na fursa yoyore ya kusonga mbele, lakini kiungo Antonin Barak alirambishwa kadi nyekundu dakika 20 za mchezo na ikavuruga mipango yao.
Ilikuwa mechi ya hisia kali na sekunde chache kabla ya kukamilika Tomas Chory wa Czech akaonyeshwa nyekundu. Pamoja na hizo kadi mbili nyekundu, refarii pia alitoa kadi 16 za njano na kuweka historia mpya ya kinidhamu katika michuano ya Euro.
Hungary ambao wamekuwa wakisubiri katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu tangu mechi za Kundi A zilipokamilika Jumapili, sasa wamefurushwa kupitia tofauti ya mabao.
Croatia, ya tatu katika Kundi B, awali waliondolewa kwenye mnyukano huo.
Austria sasa inaisubiri Uturuki katika hatua ya mchujo Jumanne usiku wiki ijayo.