Mwili wa Malkia Elizabeth kupelekwa London
13 Septemba 2022Jeneza lenye mwili wa Malkia Elizabeth wa II aliyeaga dunia wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 96, litasafirishwa kwenda mjini London kwa ndege ya kikosi maalum cha jeshi baada ya kukamilika siku mbili za kutoa heshima za mwisho huko Scotland.
Mtoto wa kike wa Malkia Elizabeth Anne ndiye pekee atausindikiza mwili wa mama yake kwenda London kama alivyofanya wakati ulipotolewa kutoka kasri la Balmoral na kupelekwa mjini Edinburgh siku ya Jumapili.
Ratiba kuelekea mazishi yatakayofanyika Septemba 19 inaonesha mwili wa Malkia Elizabeth utawekwa kwenye hekalu la Westminster kuanzia siku ya Jumatano na waombolezaji watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho.
Maelfu ya watu tayari wameanza kupanga foleni ya kutoa heshima za mwisho siku mbili kabla ya tukio hilo. Ratiba inaonesha umma utakuwa na muda wa siku nne za kupita mbele ya jeneza kumuaga Malkia Elizabeth.
Maelfu ya watu watoa heshima za mwisho kwa Malkia huko Scotland
Usiku kucha wa kuamkia leo maelfu ya watu walijitokeza kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Malkia Elizabeth uliokuwa umewekwa ndani ya kanisa kuu la Mtakatifu Giles mjini Edinburgh.
Wengi ya waombolezaji walionekana kububujikwa machozi walipokuwa wakipita mbele ya jeneza hilo lililofunikwa kwa bendera ya ufalme wa Uingereza na pembeni yake kukiwa na taji lililonakshiwa kwa vito vya thamani.
Mmoja ya waombolezaji waliopata nafasi ya kutoa heshima za mwisho amesema, "Ni huzuni. Nashindwa kuamini kuwa ametutoka. Kwa sababu ilikuwa ghafla sana, ninashindwa kuamini. Kwa hivyo ilikuwa muhimu kuwa pamoja na familia, na tumekuja hapa, kumuaga".
Jana jioni kulikuwa na tukio la kuwasha mishumaa ambapo Mfalme Charles wa III alijiunga na ndugu zake kuongoza tukio hilo mbele ya jeneza lenye mwili wa mama yao.
Mfalme Charles akiwa pamoja na dada yake Anne, mwanamfalme Andrew na mtoto wa mwisho wa Malkia Elizabeth mwanamfalme Edward waliomboleza kwa kufumba macho kwa muda wa kiasi dakika kumi.
Mfalme Charles wa III kiuzuru Ireland Kaskazini kuongoza maombolezo
Wakati huo huo Mfalme Charles wa III hii leo atafanya ziara Ireland ya Kaskazini na kisha kuitembelea Wales siku ya Ijumaa kwa lengo la kujitambulisha rasmi baada ya kutawazwa kuwa mfalme wa Uingereza.
Alikwishafanya hivyo huko Scotland ambako alikutana na viongozi wa kisiasa ikiwemo waziri kiongozi Nicola Sturgeon.
Maelfu ya watu wanatazamiwa kumkaribisha mfalme Charles huko Ireland Kaskazini ambako atakutana na viongozi wa kisiasa na kisha kuhudhuria ibada ya misa mjini Belfast.
Hata hivyo ziara hiyo itagubikwa na kiwingu cha mvutano wa kisiasa unaoendelea Ireland Kaskazini kati ya wale wanaopendelea eneo hilo kubakia ndani ya Uingereza na wale wanaotaka lijiunge na Jamhuri ya Ireland.