Malkia Elizabeth II afariki dunia
8 Septemba 2022Malkia Elizabeth II wa nchini Uingereza amefariki dunia. Malkini Elizabeth anatajwa kama kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini humo na kuipitisha Uingereza katika nyakati ngumu na nyepesi katika kipindi chote cha utawala wake wa miaka 70. Malkia amefariki akiwa na miaka 96.
Kasri ya Buckingham imetangaza kwamba Malkia amefariki akiwa katika kasri ya Balmoral huko Scotland ambako huwa anapumzika katika majira ya joto. Tangu mchana familia ya kifalme ilianza kukusanyika kwenye kasri hiyo, baada ya taarifa kutolewa kwamba malkia alikuwa chini ya uangalizi wa matabibu wake kwa kuwa hali yake kiafya ilikuwa imedhoofika mno.
Mwanae Prince Charles mwenye miaka 73 ndio anakuwa mfalme, ingawa kuthibitishwa kwake kunaweza kuchukua miezi kadhaa. Haijulikani iwapo atajiita Mfalme Charles III ama atajiita majina mengine.
Shirika la habari la Uingereza BBC, lilirusha wimbo wa taifa wa "God Save the Queen" huku likionyesha picha nzima ya malkia baada ya kutangazwa kwa taarifa hizo za kifo na bendera katika kasri ya Buckingham ilishushwa hadi nusu mlingoti.
Athari za kifo chake zinatarajiwa kuwa kubwa na zisizopimika, sio tu kwa Uingereza bali pia kwa ufalme wenyewe, ambao amekuwa akiusimamia kwa uthabiti kwa miongo yote saba aliyotawala, katika nyakati ambazo ulikumbwa na misukosuko na hata kashfa.
Mapema, ilitangazwa kwamba Malkia Elizabeth aliwekwa chini ya uangalizi wa madaktari katika kasri ya Balmoral huko Scotland, siku moja baada ya Malkia kufuta mkutano kwa njia ya mtandao na baraza lake la ushauri wakati madaktari wake walipomshauri siku nzima ya leo kupumzika, baada ya siku ya Jumanne pia kuwa na shughuli nzito ya kumuteuwa rasmi Liz Truss kuwa waziri mkuu katika kasri ya Balmoral, Scotland.
Prince Charles, mrithi wa kiti cha ufalme, pamoja na mkewe Camilla na dada yake Anne walikuwa pamoja na Malkia kwenye kasri ya Balmoral, ambako hupumzika wakati wa majira ya joto.
Malkia Elizabeth alipokea kijiti cha utawala baada ya kifo cha baba yake Februari 6, 1952 na tangu wakati huo amechukuliwa kama nembo ya uthabiti na kujenga mahusiano na ushirikiano ndani na nje ya Uingereza.
Katika siku za karibuni Malkia Elizabeth amekuwa akikabidhi majukumu kwa Charles na wanafamilia wengine na hasa baada ya kupata maambukizi ya virusi vya COVID-19.