1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier: Kushindwa kwa utawala wa Manazi ni ukombozi

8 Mei 2020

Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amesema Wajerumani wanashukuru kushindwa kwa utawala wa Manazi ambao ulimaliza Vita Kuu ya Pili ya Dunia barani Ulaya miaka 75 iliyopita.

https://p.dw.com/p/3bwju
75. Jahrestag Ende zweiter Weltkreig - Frank Walter Steinmeier
Picha: Reuters/H. Hanschke

Steinmeier ameitoa kauli hiyo Ijumaa wakati wa kuadhimisha kumbukumbu hiyo. Akihutubia katika kumbukumbu ya miaka 75 tangu kumalizika Vita Kuu ya Pili ya Dunia mjini Berlin, Steinmeier amesema kitendo cha Ujerumani kushindwa ni cha ukombozi.

"Ndiyo, leo sisi Wajerumani tunaweza kusema siku ya ukombozi ni siku ya shukrani. Ilichukua miongo kadhaa kabla Ujerumani hatujalikubali hili kwa moyo wetu wote," alifafanua Steinmeier.

Maneno ya rais wa zamani

Matamshi ya Steinmeier yalikumbushia hotuba ya rais wa zamani wa Ujerumani, Richard von Weizsaecker aliyoitoa mwaka 1985 na kuwa mtu wa kwanza kuwataka Wajerumani kuikumbuka Mei 8 kama sio tu kama siku ya kushindwa, lakini pia siku ya ukombozi kutoka kwa utawala wa kidhalimu wa Manazi.

Steinmeier na Kansela Angela Merkel waliweka mashada ya maua kwenye eneo la kumbukumbu la wahanga wa vita na utawala wa kidikteta la Neue Wache, mjini Berlin.

Steinmeier ameelezea masikitiko yake kwamba wawakilishi wa nchi washirika zilizoudondosha utawala wa Manazi Ujerumani pamoja na maelfu ya vijana kutoka ulimwenguni kote ambao walialikwa katika maadhimisho hayo, wameshindwa kuhudhuria kwa sababu ya janga la virusi vya corona.

75. Jahrestag Ende zweiter Weltkreig - Angela Merkel, Wolfgang Schäuble und Frank Walter Steinmeier
Kansela Angela Merkel, Spika wa Bunge la Ujerumani, Wolfgang Schäuble na Rais Frank-Walter Steinmeier wakiweka mashada ya mauaPicha: Reuters/H. Hanschke

Amesema Ujerumani ina jukumu la kuifanya Ulaya kuwa moja kutokana na matokeo ya historia yake, hasa wakati huu wa mzozo wa COVID-19.

Mjini Warsaw, Poland, Rais Andrzej Duda amesema kumbukubmu hii inaonyesha kumalizika kwa mateso ya wakati wa vita, kulifuatiwa na Poland kuangukia kwenye ushawishi wa Kisovieti.

Hotuba ya Malkia

Nchini Uingereza maadhimisho hayo yalihusisha gwaride karibu na kasri la Malkia, lakini shughuli nyingi ziliahirishwa au kufutwa kabisa. Baadae usiku vituo vya televisheni vya Uingereza vitarusha hotuba ya Malkia Elizabeth wa Pili.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameongoza maadhimisho hayo katika uwanja wa ushindi wa Arc de Triomphe mjini Paris, yaliyohudhuriwa na maafisa waandamizi wa jeshi pekee.

Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern alitoa heshima zake kwa maveterani wa nchi hiyo pamoja na mashujaa na waliojitoa wakati wa vita hivyo.

Rais wa Urusi Vladmir Putin leo amezungumza na Kansela Merkel kwa njia ya simu katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo na wamekubaliana kwamba vita ni ukumbusho haja ya kuwepo ushirikiano wa karibu zaidi kati ya mataifa na watu ili kuhimiza amani na maelewano.

(AFP, AP, DPA, Reuters)