1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamuziki mwingine maarufu afariki jela nchini Rwanda

Saleh Mwanamilongo
2 Septemba 2021

Mwanamuziki Jay Polly amefariki leo Alhamisi akiwa gerezani. Polly ni mwanamuziki wa pili kuzuiliwa na kufariki katika jela katika mazingira ya kutatanisha.

https://p.dw.com/p/3zpoL
Afrika Uganda l Katuna - Grenze zu Ruanda
Picha: DW/A. Gitta

Polly,ambaye jina lake halisi ni Joshua Tuyishime,alikuwa anashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na  dawa za kulevya na kesi yake ilitakiwa kufunguliwa tarehe Mbili Desemba.

Pascal Nkubito, Mkuu wa Hospitali ya Muhima,mjini Kigali ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kijana huyo wa miaka 33 alikuwa katika hali mahututi na hakuzungumza wakati alipofikishwa kwenye hospitali hiyo mapema leo asubuhi. Amesema madaktari walijaribu bila mafanikio kuokoa maisha yake na alifariki muda mfupi baadaye.

Nkubito amesema sababu ya kifo hicho haifahamiki hadi baada ya uchunguzi wa maiti. Mwanamuziki huyo wa muziki wa aina ya kufokafoka au Rapp alikamatwa nyumbani kwake mnamo Aprili kwa madai ya kuandaa sherehe kinyume na kanuni za kupambana na Covid-19 zilizowekwa nchini Rwanda. Baadaye akaonyeshwa pamoja na washukiwa wengine mbele ya vyombo vya habari.

Mushtuko nchini Rwanda

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Rwanda wameomboleza kifo cha Jay Polly
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Rwanda wameomboleza kifo cha Jay Polly Picha: DW

Polisi ilisema Tuyishime na washtakiwa wengine walipatikana wakinywa pombe na wakiwa na bangi na vyeti bandia vya Covid-19. Polly alikanusha tuhuma hizo lakini maombi yake ya kuachiwa kwa dhamana yalikataliwa.

Taarifa ya kifo chake imepokelewa kwa mshtuko mkubwa nchini Rwanda. John Willians Ntwali ni mwanamuziki kutoka Rwanda.

''Kusikia kwamba amefariki ni mshtuko mkubwa.Kwa sababu ni miongoni mwa wanamuziki mashuhuri sana wa kizazi kipya hapa nchini Rwanda'', alisema Ntwali.

Mwanamuziki wa pili kufariki jela

 Kizito Mihigo ambaye polisi ilisema alijinyonga akiwa rumande
Kizito Mihigo ambaye polisi ilisema alijinyonga akiwa rumandePicha: Getty Images/S. Aglietti

Raia wa Rwanda walitumia mtandao wa Twitter kutoa maoni yao kuhusu kifo hicho cha Tuyishime, na baadhi ya  maoni hayo yakimtaja kama nguli wa muziki wa tamaduni ya Rwanda. Mnamo Februari mwaka jana,Kizito Mihigo, ambaye muziki wake ulipigwa marufuku na utawala wa Rais Paul Kagame,alikutwa amekufa ndani ya seli yake, siku chache tu baada ya kunaswa akijaribu kukimbia nchi.

Polisi ilisema Mihigo, aliyenusurika mauaji ya kimbari ya Rwanda na ambaye nyimbo zake za injili ziliikasirisha serikali ya Kagame,ilidaiwa  alijiua kwa kujinyonga kwenye dirisha la seli yake akitumia shuka.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch,miongoni mwa mashirika mengine, yameushutumu utawala wa Kagame kwa kukamatwa kwa watu kinyume cha sheria na kuteswa wakiwa chini ya ulinzi.