1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda: Miezi 6 tangu kufa Kizito Mihigo haki haijapatikana

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
18 Agosti 2020

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limesema nusu mwaka umeshapita tangu Kizito Mihigo, msanii maarufu nchini Rwanda afariki wakati akiwa mahabusu, lakini mpaka sasa haki haijatendeka.

https://p.dw.com/p/3h8mi
Kizito Mihigo Ruanda Musiker Sänger
Picha: Getty Images/C. Ndegeya

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na shirika la kutetea haki za binadamu - Human Rights Watch, maafisa wa Rwanda waliripoti kwamba hayati Kizito Mihigo aliyekuwa mwanamuziki mashuhuri nchini humo alikufa wakati  akiwapo kwenye kituo cha polisi cha Remera. Maafisa hao walidai kwamba Mihigo alijiua kwa kujinyonga.

Hata hivyo siku chache kabla ya hapo Mihigo alilijulisha shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch kwamba maisha yake yalikuwa hatarini. Alitakiwa atoe ushahidi wa uongo dhidi ya wapinzani na kwamba alikuwa anataka kukimbia kutoka nchini Rwanda kutokana na usalama wake kutishiwa. Mwanamuziki huyo alikuwa na hofu kubwa ya kuuliwa na mawakala wa serikali. Hapo awali alifungwa kwa muda wa miaka minne kwa sababu ya kuikosoa serikali.

Marehemu Kizito Mihigo akizungumza na waandishi wa habari mnamo mwaka 2014
Marehemu Kizito Mihigo akizungumza na waandishi wa habari mnamo mwaka 2014Picha: Getty Images/S. Aglietti

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema kuwa lilimwandikia barua Waziri wa Sheria wa Rwanda Johnston Busingye mnamo Agosti 10 kuomba taarifa zinazohusu uchunguzi uliokwisha fanywa kuhusu kifo cha kutatanisha cha Kizito Mihigo wakati akiwa kizuizini lakini halijapata majibu mpaka sasa. Limesema sasa ni wajibu wa serikali ya Rwanda kuthibitisha kwamba Mihigo hakuuliwa wakati akiwamo mahabusu. Hata hivyo mpaka sasa serikali hiyo haijachukua hatua yoyote na badala yake inadai kwamba mtu huyo alijiua kwa kujinyonga.

Inadaiwa kuwa Kizito Mihigo alikamatwa katika eneo la Nyaruguru karibu na mpaka wa Burundi mnamo mwezi Februari. Alikuwa na wenzake wengine wawili. mwanamuziki huyo alikamatwa kwa madai kwamba alikuwa anavuka mpaka kinyume cha sheria ili kwenda kujiunga na waasi. Mahakama kuu ya Rwanda ilimhukumu kifungo cha miaka 10 mnamo mwaka 2015, kwa kupatikana na hatia ya kuwa na uhusiano magenge ya uhalifu. Hata hivyo aliachiwa mwaka 2018 kutokana na msamaha wa rais. 

Upande wa mawakili wa serikali umesema polisi wa zamu, siku hiyo hakusikia chochote cha kusumbua na wamebainisha  kwamba alikufa kutokana na ukosefu wa hewa, yumkini alijinyonga. Shirika la kutetea haki za binadamu limesema hata hivyo wahusika nchini Rwanda walipaswa kuruhusu uchunguzi huru ili kuthibitisha taarifa yao juu ya kifo cha Mihigo.

Katika taarifa ya kwa vyombo vya habari shirika la kutetea haki za binadamu - Human Rights Watch limesema uchunguzi na mashtaka ni muhimu na ni msingi wa kuzuia ukiukaji wa haki za maisha ya watuhumiwa, kukuza uwajibikaji pamoja na kutii sheria na kushindwa kuheshimu jukumu la uchunguzi ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Chanzo: HRW

Mwandishi: Zainab Aziz