Mwanamuziki mashuhuri Rwanda Kizito Mihigo ajinyonga
17 Februari 2020Habari za kufariki dunia kwa kujinyonga kwa mwanamuziki huyu aliyegeuka kuwa mwanasiasa zimefahamika punde majira ya saa za asubuhi. Kizito alikuwa amekaa siku tatu kwenye kizuizi cha polisi baada ya kukamatwa kwenye kile polisi walichodai ni jaribio kutorokea nchini Burundi kupitia upande wa kusini mwa nchi ili kujiunga na makundi yenye silaha.
Tangazo lililotolewa na polisi ya Rwanda limesema na hapa ninakuu "Leo majira ya alfajiri saa kumi na moja Kizito Mihigo mwenye aliyekuwa na umri wa miaka 38 aliyekuwa akizuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Remera mjini Kigali amekutwa amejinyonga na kufariki dunia."
Tangazo hilo liliendelea kusema kuwa Kizito alikuwa amemaliza "siku tatu akizuiliwa kwenye kituo hicho kwa shutuma za kosa la kujaribu kuvuuka mipaka ya nchi kinyume cha sheria pamoja na kujaribu kutoa rushwa."
Mwanamuziki huyu kwa mara ya kwanza alikamatwa mwaka 2015 na kuhukumiwa kifunga cha miaka kumi jela baada ya kukutikana na hatia ya kushirikiana na makundi yenye silaha yaliyokuwa na nia ya kuipindua serikali ya Rwanda.
Wakosoaji wahoji usalama wa vizuizi vya polisi kwa mahabusu
Lakini mwaka 2018 akaachiwa huru kwa msamaha wa Rais Paul Kagame akiwa pamoja na wafungwa wengine 2,140 - akiwemo mwanasiasa mpinzani wa serikali ya Rwanda mwanamama Victoire Ingabire kiongozi wa chama kisichokubalika kisheria nchini Rwanda cha FDU Inkingi.
Baadhi ya wadadisi wamekuwa na maoni kuhusu kifo cha mwanamuzi huyu.
"Ni taarifa ambayo tumeipokea kwa mshangao mkubwa kwasababu, Kwanza alikuwa bado ni kijana mdogo kiumri, miaka 38 alivyokamatwa mara ya kwanza, tulishangaa kwanza kuona msanii anajihusisha na mambo ya ksisasa kiasi hicho, lakini baada ya , kupema msamaha na rais pia hatukutegemea kama atarudia kosa, lakini tumeona wote kwamba amerudia kosa, kwahiyo baada ya kukamatwa kwa mara ya pili nafikiri akasema hapa ndio mwisho wa maisha yangu" alisema mmoja ya mchambuzi nchini Rwanda
Hata hivyo, kitendawili ni kwamba tangazo la polisi pia limesema amejiua siku mbili baada ya marafiki na jamaa zake kumtembelea kwenye kizuizi cha polisi.
Wale waliokataa kunaswa sauti zao wamehoji usalama wa vizuizi vya polisi kwa mahabusu kwa kuzingatia kila mahabusu anayeingia hupekuliwa na vitu vyote kusalia nje.
Hilo ni swali ambalo lingejibiwa na msemaji wa jeshi la John Bosco Kabera ambaye hakuweza kupatikana na mara moja.
Chanzo: Sylivanus Karemera/DW Kigali