1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asili na mazingiraSaudi Arabia

Mvua kubwa yasababisha maafa katika mataifa mengi duniani

17 Aprili 2024

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dubai, umewashauri abiria kutosafiri kuelekea eneo hilo kama sio lazima baada ya mji huo wa UAE kukumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko

https://p.dw.com/p/4esSZ
Watu wanatazama mafuriko kwenye barabara moja kuu mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu Jumatano Aprili 17,2024
Mafuriko kwenye barabara moja kuu mjini Dubai katika Umoja wa Falme za KiarabuPicha: Jon Gambrell/AP/dpa/picture alliance

Kulingana  na data ya idara ya hali ya hewa iliyokusanywa katika uwanja huo wa ndege wa kimataifa, mvua hiyo ilianza kunyesha siku ya Jumatatu jioni. Mvua hiyo iliongezeka mwendo wa saa tatu asubuhi jana Jumanne na kuendelea kunyesha siku nzima .

Paul Griffiths, mkurugenzi mkuu wa uwanja huo wa ndege, amethibitisha leo kutokea kwa mafurikohayo na athari zake na kuongeza kuwa kila mahali ambapo ndege zingeweza kuegeshwa salama pamejaa maji ya mafuriko hayo.

Griffiths asema hali katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dubai ni ngumu

Griffiths amekiambia kituo cha redio cha serikali, Dubai Eye kwamba baadhi ya ndege zimeelekezwa katika uwanja wa ndege wa pili wa kimataifa wa Al Maktoum mjini humo na kuongeza kuwa huu ni wakati mgumu na ni hali ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.

Soma pia:Je mabadiliko ya tabia nchi yamechangia mafuriko?

Hata hivyo amesema wanafanya bidii kuhakikisha wateja na wafanyakazi wanashughulikiwa vilivyo.

Shule katika Umoja wote wa Falme za kiarabu, kwa kiasi kikubwa zilifungwa kabla ya mvuahiyo kubwa na wafanyakazi wengi wa serikali kufanyia kazi majumbani.

Mafuriko mtoni Charsadda mjini Peshawar nchini Pakistan, Aprili 15,2024
Mafuriko mjini Peshawar nchini PakistanPicha: Hussain Ali/Zuma/IMAGO

Mvua pia ilinyesha katika nchi za Bahrain, Oman, Qatar na Saudi Arabia.

Watu 63 wafariki dunia kutokana na mafuriko nchini Pakistan

Nchini Pakistan, mvua kubwa na radi zimesababisha vifo vya watu 14. Haya yamesemwa leo na maafisa wa serikali na kufikisha idadi jumla ya waliofariki dunia kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa ndani ya siku nne kufikia takriban watu 63 huku mvua hiyo kubwa kuwahi kunyesha katika muda wa miongo kadhaa ikisababisha mafurikokwenye vijiji vilivyoko katika Pwani ya Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.

Vifo vingi vimeripotiwa katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa ulioko Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo unaopakana na Afghanistan.

Nchini Kazakhstan, takriban watu 117,000 walihamishwa kutokana na mafuriko. Haya ni kulingana na wizara ya kushughulikia hali za dharura.

Baadhi ya watu wameanza kurejea katika makazi yao

Katika taarifa hii leo, wizara hiyo imesema kuwa takriban watu 16,000 tayari wamerejea katika makazi yao wakati maji yakipungua kwenye  baadhi ya mikoa, lakini uhamishaji bado unaendelea katika maeneo ya Kazakhstan Kaskazini, Aktobe na Kazakhstan Magharibi.

Mto Tobol nchini Urusi wafikia viwango hatari

Nchini Urusi, kiwango cha maji katika mto Tobol ulioko karibu na mji wa Kurgan kwenye eneo la Kusini la Urals kilizidi kiwango cha hatari. Haya yametangazwa leo na  shirika la habari la serikali RIA, lililonukuu mamlaka ya eneo hilo.

RIA imeripoti kuwa zaidi wa nyumba za makazi 660 zimekumbwa na mafuriko katika eneo hilo kufikia leo asubuhi.