Waathirika wa mafuriko Tanzania wahitaji msaada wa haraka
11 Aprili 2024Kuanzia wanasiasa, makundi yanayofuatilia ustawi wa jamii pamoja na wananchi wengine wa kawaida wamekuwa wakipaza sauti kutaka misaada ya haraka kuwafikia waathirika hao ambao baadhi yao wanaonyesha kukata tamaaa kutokana na mazingira wanayopitia.
Bado haijafahamika mara moja ni lini hali itatengamaa katika maeneo hayo na tayari serikali imesema imeanza kutuma watendaji wake kukagua uharibifu uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Hadi sasa wilaya nne zimefunikiwa na maji, na Waziri Mkuu Majaliwa anasema kutokana na uharibifu huo kuwa mkubwa, mawaziri kadhaa wamefunga safari kwenda kupinga kambi katika maeneo yaliyoathirika kwa ajili ya kufanya tathmini na kisha kubainisha mahitaji yanayopaswa kuzingatiwa.
Takriban watu 47 wamekufa Tanzania kufuatia maporomoko ya ardhi
Samia asema serikali itaendelea kutoa msaada kwa waathirika
Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa waathirika wa majanga hayo, na wakati alipokuwa akizungumza katika sherehe za Baraza la Eid Ul Fitr aliwahakikishia wakazi wa maeneo hayo kuwa serikali itaendelea kunyosha mkono wake ili kuwanusuru katika hali wanayokumbana nayo.
Hayo yanajiri huku mamlaka ya hali ya hewa nchini(TMA) ikionya kuhusu mvua kubwa inayotarajia kunyesha kuanzia kesho Ijumaa katika mikoa 14 na hivyo kuashiria uwezekano wa kutokea mafuriko na uharibifu katika maeneo mengi.
Mamlaka hiyo imesema mvua hizo zitanyesha katika kipindi cha siku tatu mfululizo na kwamba upo uwezekano na kushuhudia maafa katika baadhi ya maeneo.
Mwandishi: George Njogopa DW Dar es Salaam