Mafuriko yawaacha maelfu bila makaazi Kongo
19 Februari 2024Mvua kubwa iliyonyesha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, iliwalazimisha watu wapatao 500,000 kuyakimbia makazi yao kutokana na mafuriko.
Katika kambi ya muda inayowahifadhi watu waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko hayo iliyopo viungani mwa mji mkuu Kinshasa, Cyprien Seka baba wa watoto watatu anamtazama kwa wasiwasi mtoto wake akilala kwenye sakafu katika hema lililojaa watu huku akijiuliza ikiwa ingekuwa salama kwake kurejea nyumbani.
Amesema ni takriban mwezi mmoja sasa tangu waondoke katika makaazi yao kutokana na mafuriko, na sasa wanaishi maisha ambayo ni magumu chini ya hifadhi ya wasamalia wema.
"Naishi hapa na watoto na mke wangu katika kituo hiki cha kanisa katoliki ambacho kilikubali kutupa hifadhi, lakini tunateseka." Alisema Seka.
Soma pia:Hali ya usalama yaendelea kuzorota Goma
Madhila hayo yanazikumba familia nyingi katika kambi hiyo inayowapokea watu karibu 2,400 wanaoishi katika msongamano huku wengine wakilazimika kulala nje kutokana na ukosefu wa nafasi katika mahema.
Pansel Motopamba, bibi mwenye umri wa miaka 55 na anaeishi katika kambi hiyo anasema hali huwa ya kutisha majira ya usiku huku akisema kwamba kuna msongamano mkubwa watu, jambo linalopelekea watu kupata matatizo ya kupumua.
Vifo pia vimesababishwa na mafuriko hayo
Serikali ya Kongo na shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF wanasema mikoa 16 kati ya 26 nchini Kongo inakabiliana na hali hii ya mafuriko ambayo yamekwisha sababisha vifo vya watu 221 na kuharibu makumi ya maelfu ya nyumba, huku jamii za maeneo hayo zikiwa hatarini kutokana na kitisho cha kuongezeka kwa magonjwa kama malaria na typhoid.
Raphaël Tshimanga, mtaalamu wa masuala ya maji katika Chuo Kikuu cha Kinshasa anasema mji mkuu huo wa Kongo unakabiliwa na kitisho kikubwa cha mafuriko:
"Hofu ni kubwa kwa jiji la Kinshasa ambalo hupokea maji yote yanayowasili kutoka katika bonde la Kongo. Yaani kila tone la mvua zinazonyesha Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Congo-Brazzaville, Angola, Zambia na Tanzania ambazo ni nchi zilizo karibu na bonde la Kongo. Kwa hiyo, mfereji unaopitia Kinshasa unapokea kwenye usawa wa mto huo, mtiririko wote wa maji hayo."
Kulingana na shirika la Global Forest Watch, mwaka 2022 Kongo ilikuwa ikishikilia nafasi ya pili duniani baada ya Brazil kwa kiwango cha juu cha kupoteza miti.
Soma pia:Raia katika miji ya Sake, Maalehe na Kashaki wakimbilia katika mji wa Goma
Hali hii huzidisha hatari ya kutokea mafuriko kwa sababu matawi na mizizi ya miti husaidia katika kunasa maji ya mvua na hivyo kupunguza kiwango cha maji yanayotirika kuelekea mitoni.
Mafuriko zaidi nchini humo yanaweza kuwaweka hatarini watu karibu milioni 83 wanaoishi karibu na mto mkubwa katika bonde la Kongo.