Msomali anaepambania elimu ya uraia ashinda tuzo ya UN
28 Novemba 2023Abdullahi Mire mwenye umri wa miaka 36 amepongezwa kwa kupigania haki ya kupata elimu kwa kusambaza vitabu 100,000 kwa watoto walioko katika kambi zilizofurika wakimbiziza Daadab nchini Kenya.
Kwenye mahojiano na shirika la habari la AFP, Mire alisema "kitabu kinaweza kubadilisha mustakabali wa mtu, ninataka kila mtoto mhamiaji apate fursa wa kupata elimu”.
Akitangaza mshindi wa tuzo hiyo, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wahamiaji Filippo Grandi alimtaja Mire kuwa uthibitisho hai "kwamba mawazo ya kuleta mabadiliko yanaweza kutoka miongoni mwa jamii za wahamiaji”.
Mire alizaliwa nchini Somalia. Lakini kutokana na machafuko ya nchi hiyo, wazazi wake walikimbilia Kenya alikiwa bado mtoto.
Soma pia:UN: Watu 450,000 wameyakimbia mapigano mashariki mwa DRC
Kwa miaka 23, aliishi Daadab, kambi kubwa ya wakimbizi inayowahifadhi takriban watu 370,000, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Idadi hiyo ikiwa imepindukia kupita kiasi idadi cha watu 90,000 pekee wanaopaswa kuishi hapo.
Kinyume na kile UNHCR ilieleza kama "matatizo makubwa", Mire hakumaliza tu masomo yake ya msingi na sekondari katika kambi hiyo, bali pia alifanikiwa kuhitimu shahada ya uandishi wa habari na mahusiano ya umma.
Akapata nafasi ya kuishi Norway kabla ya kurudi tena Kenya. Amesema kuna kitu kilimshawishi kuwa anaweza kuwa na athari Chanya zaidi akiwa Nairobi kuliko Oslo.
Safari ya kupeleka elimu na vitabu kwa wakimbizi
Wakati mmoja akifanya kazi kama mwandishi habari kuangazia hali ya wahamiaji katika kambi ya Daadab nchini Kenya, msichana mmoja kwa jina Hodan Bashir Ali alimuomba amnunulie kitabu cha Baolojia.
Hodan alitamani kuwa daktari. Lakini katika shule yao, kitabu kimoja kingetumiwa na wanafunzi 15.
Mire amesema alimnunulia Hodan kitabu hicho na sasa ni muuguzi ambaye amesajiliwa lakini ndoto yake ya kuwa daktari ingalipo.
Kulingana na Mire kitabu hicho kilifungua mlango kwa Hodan, jambo linalotia moyo.
Mire aliamua kuanzisha shirika la elimu kwa vijana wakimbizi kuongeza ufahamu kuhusu mahitaji ya kielimu ya wakimbizi na kutafuta michango ya vitabu.
Hadi sasa shirika hilo linaloongozwa na wakimbizi, limesambaza vitabu 100,000 kwenye kambi, na limefungua maktaba tatu.
Mpango huo tayari umeongeza idadi ya vijana wanaojiunga na vyuo kupata elimu ya juu miongoni mwa wakimbizi.
Mire amesema, unaposoma kitabu, ni kama unazuru ulimwengu na kwa watu wanaozongwa na machafuko na vita waliovikimbia, vitabu ni njia bora kwao kupona.
Ameongeza pia kuwa vitabu vinahusu utoaji fursa ya kuwa na ndoto na kuwaza kuhusu kazi, na jinsi ya kuwa raia mwema katika ulimwengu wetu.
Soma pia:Kenya: Hali mbaya ya kiutu kambi ya Dadaab baada ya mafuriko
Tuzo ya Nansenhutolewa kila mwaka na mshindi hupokea medali na kitita cha dola 100,000 ambazo huwekezwa tena katika miradi ya kibinadamu.
Mwaka uliopita, tuzo hiyo ilimwendea kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel, kwa kujitolea kwake alipokuwa uongozini kulinda wahamiaji.