1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Wakimbizi wa Kipalestina wanaishi katika mazingira duni

20 Novemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu masuala ya kibinaadamu OCHA, limesema theluthi mbili ya jumla ya wakazi milioni 2.3 wa Gaza hawana makazi.

https://p.dw.com/p/4ZEAH
Gazastreifen Rafah | Lebensmittelverteilung
Raia wa Palestina wakigombea kupata msaada wa chakula huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza: 08.11.2023Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

OCHA imesema watu wapatao 900,000 waliolazimika kuyahama makazi yao kutoka kaskazini hadi kusini mwa Gaza sasa wanapewa hifadhi katika mahema ya Umoja wa Mataifa.

Shirika hilo limesema takriban watu 20,000 wameondoka kaskazini kuelekea Kusini mwa Gaza jana Jumapili, na wengi wao hulazimika kuondoka kwa mkokoteni unaoburuzwa na punda, basi au kwa miguu, na wamekuwa wakilala nje na kuishi katika mazingira duni ambapo watu 150 hutumia choo kimoja.

Israel imekuwa ikitekeleza usitishwaji mapigano kwa muda kwa sababu za kibinadamu ili kuwezesha wakaazi kusafiri kwa wakati maalum na kuelekea eneo la kusini. OCHA imesema watu hao hutumia barabara ya Salah-al-Din kati ya saa moja asubuhi na kumi jioni.

Soma pia: Uhaba wa mafuta watatiza shughuli za kiutu Gaza

Tangu kuanza kwa mzozo huu Oktoba 7 ambapo wanamgambo wa Hamas walivamia Israel na kuua watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine 240 kulingana na taarifa za Israel, wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na kundi la Hamas imesema mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yamesababisha yamepelekea hadi sasa watu 13,000 kuuawa huku 5,500 miongoni mwao wakiwa ni watoto.

Mashambulizi katika hospitali za Gaza

Gazastreifen | Neugeborene aus dem Al Schifa Krankenhaus nach Rafah evakuiert
Muuguzi akiwapa matibabu watoto njiti (waliozaliwa kabla ya wakati) waliosafirishwa kutoka hospitali ya Shifa na kuelekea Misri kupitia kivuko cha Rafah: 19.11.2023Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Mashambulizi hayo katika hospitali yamevuruga kabisa mfumo wa afya. Watoto 28 waliozaliwa kabla ya wakati wameondolewa katika Hospitali ya al-Shifa huko Gaza na kusafirishwa leo hii kupitia kivuko cha Rafah ili waweze kupewa matibabu nchini Misri. Hayo ni kulingana na Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin, Ujerumani wakati akihudhuria kongamano la wawekezaji chini ya mpango wa ushirikiano kati ya bara la Afrika na mataifa yaliyoendelea kiviwanda ya G20, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Comoro Azali Assoumani amesema:

" Kwa hakika, vitendo vya Hamas ni vya kulaaniwa, wale waliofanya vitendo hivyo kutoka Gaza wanakemewa, lakini jibu ambalo lilitolewa kuhusiana na kile kilichofanyika, halikubaliki."

Soma pia: Guterres: Gaza yageuka uwanja wa makaburi kwa watoto

Mamlaka za Palestina zimesema kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo huu, vifaa vya kuanzisha hospitali za dharura pamoja na wauguzi wapatao 170 kutoka Jordan wameingia katika Ukanda wa Gaza ambao unakabiliwa na idadi kubwa ya majeruhi wanaokadiriwa kufikia 30,000.

Siku ya Jumanne, kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi uliwenguni BRICS linalozijumuisha Brazil, Urusi, China, India na Afrika Kusini limeandaa mkutano wa kilele utakaofanyika kwa njia ya mtandao ili kujadili mzozo huu kati ya Israel na Hamas.