Mkuu wa ujasusi Israel ajiuzulu kufuatia shambulizi la Hamas
22 Aprili 2024Jeshi la Israel limesema hii leo kwamba mkuu wa idara ya ujasusi Meja Jenerali Aharon Haliva amejiuzulu, ikiwa ni hatua ya kuwajibika kwa kushindwa kuzuia shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Hamas nchini humo, Oktoba 7, 2023.
Meja Jenerali Aharon Haliva ni afisa wa kwanza wa ngazi za juu kujiuzulu kwa kushindwa kuzuia shambulizi hilo lililoishtua Israel pamoja na jamii ya kimataifa, na kwenye barua ya kujiuzulu, Haliva amekiri hilo.
Soma: Watu 22 wauawa kutokana na shambulizi la Israel mjini Rafah
Taarifa ya jeshi la Israel - IDF - imesema, imeafikiwa kwamba Meja Jenerali Haliva atahitimisha majukumu yake na kustaafu jeshi, baada ya mrithi wake kuteuliwa katika utaratibu wa kitaalamu.
Wanamgambo wa Hamas walifanya shambulizi kubwa kabisa nchini Israel mnamo Oktoba 7, na kusababisha vifo vya watu 1,170 na hasa raia, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za shirika la habari la AFP, zikinukuu mamlaka za Israel.
Tangu wakati huo, Israel imeapa kuliangamiza kundi la Hamas na kuanzisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo linalotawala Ukanda wa Gaza.