Watu 22 wauawa kutokana na shambulizi la Israel mjini Rafah
22 Aprili 2024Shambulizi la kwanza la Israeli mjini Rafah lilimuua mwanamume mmoja na mkewe pamoja na mtoto wao mwenye umri wa miaka mitatu. Haya ni kulingana na hospitali ya karibu na eneo hilo yaKuwaiti iliyopokea miili hiyo.
Shambulizi la pili lilisababisha vifo vya watoto 17 na wanawake wawili wa familia moja.
Wasiwasi waibuka Ukingo wa Magharibi
Wasiwasi pia umeibuka katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, ambako wanajeshi wa Israel waliwaua Wapalestina wawili ambao jeshi hilo linasema walikishambulia kituo kimoja cha ukaguzi kilichoko karibu na mji wa kusini wa Hebron mapema Jumapili.
Soma pia:Israel yaendelea kuulenga mji wa Rafah, Ukanda wa Gaza
Hata hivyo, jeshi hilo limesema kuwa hakuna mwanajeshi wake aliyejeruhiwa.
Marekani yaidhinisha msaada kwa Israel
Marekani siku ya Jumamosi iliidhinisha msaada wa dola bilioni 26 kwa Israel. Msaada huo unajumuisha dola bilioni 9 za msaada wa kiutu kwa Gaza ambao wataalamu wanasema inakabiliwa na hatari ya njaa.
Huenda bunge la seneti likapitisha msaada huo kesho Jumanne huku Rais Joe Biden akiahidi kuutia saini mara moja.
Mkuu wa idara ya ujasusi wa Israel ajiuzulu
Mkuu wa ujasusi wa Israel, Meja Jenerali Aharon Haliva, amekuwa afisa wa kwanza wa ngazi za juu nchini humo kujiuzulu kwa kushindwa kuzuia shambulizi la Hamas ambalo liliitikisa nchi hiyo na jamii ya kimataifa.
Soma pia:Marekani inaikosoa vikali Israel kuivamia Rafah
Katika taarifa, jeshi la nchi hiyo limesema kuwa Haliva, kwa mashauriano na mkuu wa majeshi, aliomba kujiuzulu kufuatia jukumu lake la uongozi kama mkuu wa idara ya ujasusi kutokana na matukio hayo ya Oktoba 7.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa ilikuwa imeamuliwa kwamba Haliva angelijiuzulu wadhifa wake na pia kutoka kwenye jeshi la nchi hiyo pindi mrithi wake wa atakapochaguliwa kupitia mchakato mwafaka na wa kitaalamu.
Soma pia:Israel yaacha uharibifu ´usio mfano´ hospitali ya Al Shifa
Katika barua yake ya kujizulu, Haliva aliyehudumu kwenye jeshi hilo kwa miaka 38, alikiri kushindwa katika majukumu yake.
Haliva ameongeza kuwa amekuwa akibeba machungu ya tukio hilo kila siku na ataendelea kubeba uchungu huo wa vita.
Haliva pia ametoa wito wa uchunguzi wa kina kuhusu masuala na hali zilizopelekea shambulizi hilo.
Scholz aonya dhidi ya kutanuka kwa mzozo wa Mashariki ya Kati
Mbali na hayo, wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hapo jana, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwa mara nyingine alionya dhidi ya kutanuka kwa mzozo katika Mashariki ya Kati.
Soma pia:Mashambulizi makali ya Israel yapiga kusini mwa Gaza, katikati ya ongezeo la kitisho cha njaa
Kulingana na msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Hebestreit, Scholz pia alielezea uamuzi wa wakuu wa nchi na mawaziri wa Baraza la Umoja wa Ulaya la vikwazo zaidi dhidi yaIran.
Hebestreit ameongeza kuwa Netanyahu alimuarifu Scholz kuhusu hali katika eneo hilo.