Mashambulizi yaendelea kurindima Gaza
28 Machi 2024Ukosoaji wa Marekani dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu umeongezeka kuhusiana na idadi ya vifo vya raia huko Gaza, uhaba mkubwa wa chakula, na mipango ya Israel kuendelea na operesheni yake dhidi ya wanamgambo wa Hamas ndani kabisa ya mji wa kusini wa Rafah, ambao umefurika raia walioyakimbia maakazi yao.
Mashambulizi na mapigano yameendelea Gazalicha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa Jumatatu likitaka usitishwaji maramoja wa mapigano na kuwachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo.
Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre amesema serikali ya Netanyahu imerudi nyuma na kukubaliana "kupanga upya mkutano wa kujadili operesheni ya Rafah”. Amesema wanashauriana kupata tarehe muafaka. "Ninachoweza kusema juu ya Israeli kwa upana zaidi, unaponiuliza kuhusu mikutano ambayo ilifanyika hapa, yalikuwa majadiliano mazuri na waziri wa ulinzi wa Israel katika siku mbili zilizopita. Kwa hiyo sasa tunafanya kazi nao kutafuta tarehe mwafaka ambayo bila shaka itazifaa pande zote mbili. Lakini ofisi ya waziri mkuu imekubali kupanga upya mkutano huo ambao utajadili Rafah, ambalo ni jambo zuri."
Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Mathew Miller amesema wanapanga kuipa Israel mbadala wa operesheni ya Rafah, unaolenga kuyapiga maeneo ya Hamas na wakati huo huo kupunguza vifo vya raia.
Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema leo kuwa watu 66 waliuawa usiku wa kuamkia leo
Mapigano yaliendelea karibu na hospitali tatu za Gaza, na kuongeza hofu kwa wagonjwa, wahudumu wa afya na watu waliochukua hifadhi ndani ya taasisi hizo. Hopsitali ya Al-Amal mjini Khan Yunis imesitisha operesheni zake baada ya raia kuondolewa.
Mapema leo, jeshi limesema wanamgambo wamekuwa wakiwafyatulia wanajeshi risasi "kutoka ndani na nje ya wodi ya wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.
Vifaru vya Israel na magari ya kijeshi pia yamekusanyika karibu na hospitali ya Nasser.
Mataifa kadhaa yameanza kudondosha msaada, huku pia njia ya baharini kutoka Cyprus ikitumika kupeleka shehena ya kwanza ya chakula.
Waziri wa ulinzi Lloyd Austin, kabla ya kukutana na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant, alisisitiza kuwa "idadi ya vifo vya raia iko juu mno, na kiasi cha msaada wa kiutu kiko chini mno huko Gaza.
Machafuko pia yameongezeka katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, ambako wahudumu wa afya na jeshi wamesema watu watatu wamejeruhiwa katika shambulizi la bunduki leo ambalo lilililenga basi la shule.
Vita hivyo vimeongeza hofu ya mzozo huo kutanuka na kuwa wa kikanda, hasa kwenye mpaka wa Israel na Lebanon. Vuguvugu la Hezbollah la Lebanon limetangaza vifo vya wanachama wake wanane baada ya makabiliano ya ya mpakani ya siku nzima na Israel kusababisha vifo vya karibu watu 16.
AFP