Mkutano wa uchumi kati ya Afrika na Saudia waanza Riyadh
9 Novemba 2023Mapema hii leo Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia Mohammed Al-Jadaan aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba Taasisi ya Mfuko wa Maendeleo ya Saudia itawekeza kiasi dola za kimarekani milioni 533 kwenye mataifa ya Afrika.
Amesema pia taifa hilo la Ghuba linafanya kazi na washirika wengine kuzisaidia Ghana na nchi nyingine za Afrika zinazoandamwa na kiwingu cha kushindwa kulipwa madeni.
Kadhalika kumetolewa ahadi nyingine ya mamilioni ya dola kutoka kwenye Mfuko wa Uwekezaji wa nchi hiyo ambapo kiongozi wa mfuko huo Khalid Al-Falih amesema uwekezaji wake utaleta mabadiliko makubwa barani Afrika.
Kwenye mkutano huo, Saudi Arabia pia imetiliana saini makubaliano ya awali ya uwekezaji kwenye sekta ya nishati na mataifa kadhaa ya Afrika ikiwemo Nigeria, Senegal, Chad na Ethiopia.