1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa mazingira COP29 waanza Azerbaijan

11 Novemba 2024

Mkutano wa kilele wa kila mwaka wa UN kuhusu mazingira, umeanza leo nchini Azerbaijan huku nchi zikijiandaa kwa mazungumzo magumu kuhusu ufadhili na biashara, kufuatia mwaka uliogubikwa na majanga ya hali ya hewa .

https://p.dw.com/p/4mrv6
mkuu wa sera ya mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa COP 29 mjini Baku, Azerbaijan mnamo Novemba 11,2024
Mkuu wa sera ya mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon StiellPicha: Alexander Nemenov/AFP

Mkutano huo wa kilele wa COP29 ulifunguliwa kwa wito kutoka kwa mkuu wa sera ya mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell, kwamba sasa ndio wakati wa kuonesha kuwa ushirikiano wa kimataifa haujagonga mwamba.

Stiell alizionya nchi tajiri zinazojivuta kukubaliana na lengo jipya la ufadhili kuachana na wazo lolote kwamba ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni hatua ya msaada.  Stiell ameongeza kuwa lengo lolote madhubuti la ufadhili wa hali ya hewa ni kwa maslahi binafsi ya kila taifa, ikiwa ni pamoja na mataifa makubwa na tajiri zaidi.

Rais wa COP anayeondoka asema historia itawahukumu kwa vitendo na sio maneno

Wakati wa kupokezana urais wa mkutano huo wa COP kwa rais wa sasa wa COP29, Mukhtar Babayev, ambaye pia ni waziri wa Ikolojia na Maliasili wa Azerbaijan, Rais anayeondoka, Sultan Al Jaber, amesema kuwa makubaliano waliyoyapata Dubai yalikuwa ya kihistoria na akamtaka mrithi wake kuhakikisha kuwa vitendo vinaonekana zaidi ya maneno.

Babayev athibitisha mahitaji ya ufadhili ni makubwa

Wakati huo huo, Babayev alithibitisha kuwa mahitaji ya ufadhili wa hali ya hewa ni makubwa sana kuliko kiwango ambacho kinaweza kupatikana kwenye uhalisia na akasema kwamba mazungumzo hapo ni tata na magumu.

Rais wa COP28 Sultan Al Jaber akiwahutubia waandishi wa habari  wakati wa mkutano wa kilele wa mazingira COP2, Dubai mnamo Desemba 4, 2023
Rais wa COP28 Sultan Al JaberPicha: Kamran Jebreili/AP

Nchi zinazoendelea nayo zimeonya kuwa bila ufadhili wa kutosha, zitatatizika kutoa sasisho madhubuti kwa malengo yao ya hali ya hewa, ambayo nchi zinatakiwa kuwasilisha mapema mwaka ujao.

Kundi la hali ya hewa la LDC latoa wito wa ufadhili zaidi

Evans Njewa, mwenyekiti wa kundi la Hali ya Hewa la mataifa yanayoendelea LDC, ambayo ni makazi ya takriban watu bilioni 1.1, ametoa wito wa ufadhili zaidi ili kudhihirishwa kwa uongozi wa mataifa yalioendelea.

Marekani yatoa ahadi ya bilioni 3 kwa mabadiliko ya tabia nchi

LDC, pia inataka kupanuliwa kwa orodha ya ufadhili kujumuisha mataifa mengine tajiri na yanayochangia zaidi katika uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na China na mataifa ya Ghuba.

Kwa mara nyingine tena, Rais mteule wa Marekani Donald Trump, ameahidi kuiondoa Marekani kwenye makubaliano ya kihistoria ya hali ya hewa ya Paris, na kuna wasiwasi kwamba hatua hiyo inaweza kudhoofisha matarajio ya mazungumzokuhusu hali ya hewa.