COP28 inazingatia kukatizwa rasmi kwa nishati ya visukuku
5 Desemba 2023Rasimu hiyo ya kile ambacho kinaweza kuwa makubaliano ya mwisho ya mkutano wa COP28, iliyochapishwa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, inaanzisha mazungumzo kuhusu kile kinachozingatiwa kuwa suala muhimu katika mkutano huo ambacho ni iwapo mataifa yatakubaliana hatimaye kuhitimisha matumizi ya nishati ya visukuku au kupigania kudumisha matumizi yake.
Hatima ya mafuta, gesi na makaa ya mawe ni suala gumu zaidi linalozungumziwa katika mkutano huo wa COP28 na mgawanyiko kuhusu hatima ya nishati hizo umedhihirika wazi katika mkutano huo.
Chaguo tatu za maamuzi yanayopaswa kufanywa
Toleo hilo la pili la rasimu hiyo ya mazungumzo linatoa chaguo tatu za maamuzi yanayopaswa kuchukuliwa na kusababisha mazingira ya mapambano makali huku wawakilishi kutoka takriban mataifa 200 wakijaribu kufikia makubaliano ya mwisho.
Chaguo la kwanza linapendekeza hatua ya taratibu na ya haki katika kusitisha matumizi ya nishati ya visukuku, huu ukiwa msimamo mkali zaidi na unaotazamwa kuwa muhimu na mataifa ya visiwa yanayokabiliwa na kitisho cha kuongezeka kwa kina cha bahari.
Soma pia:COP28: Ahadi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi hazitekelezwi ipasavyo
Chaguo la pili, linatoa wito wa juhudi za haraka katika kusitisha miradi ambayo inakosa njia ya kunasa na kuhifadhi hewa chafuzi na kupunguza kwa haraka matumizi ya nishati ya visukuku ili kufikia utoaji sifuri wa gesi ya kaboni katika uzalishaji wa nishati duniani ifikapo mwaka 2050.
Chaguo la tatu ambalo liko katika ukurasa wa 24 wa rasimu hiyo, ni kutotajwa kabisa kukatizwa kwa matumizi ya nishati ya visukuku, msimamo unaoungwa mkono na mataifa makubwa ya uzalishaji mafuta kama vile Saudi Arabia na China.
Mataifa makubwa yanapigia upatu matumizi ya mafuta na gesi
Katika mkutano huo wa COP28, wakuu wa mashirika makubwa ya mafuta wamepigia upatu matumizi ya mafuta na gesi na kutafuta kuangazia hatua rafiki kwa hali ya hewa kama vile kukata uzalishaji wa gesi chafuzi ya Methane.
Utafiti uliochapishwa leo, umeonesha kuwa utoaji wa gesi chafuzi kutokana na kuchomwa kwa nishati ya visukuku unatarajiwa kuongezeka zaidi mwaka huu, na kuzidisha mabadiliko ya tabianchi na pia kuchochea hali mbaya zaidi ya hewa.
Wanasayansi wanautaka mkutano wa COP28 kukomesha uchafuzi
Haya yanajiri wakati wanasayansi wametoa wito kwa nchi katika mkutano huo wa COP28, "kuchukua hatua sasa" kukomesha uchafuzi unaosababishwa na makaa ya mawe, mafuta na gesi.
Wanasayansi hao wameonya kuwa ulimwengu unaweza kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5 kipimo cha Celsius katika miaka saba ijayo, huku uzalishaji wa mafuta ya visukuku ukiendelea kuongezeka.