Misri, Guinea ya Ikweta zatinga robo fainali AFCON
27 Januari 2022Guinea ya Ikweta na Mali zote zilikosa mikwaju miwili kati ya mitano ya kwanza, na beki wa Mali Falaye Sacko akakosa mkwaju wa 16 wa penalti ambao uliokolewa na mlinda mlango wa Guinea ya Iketwa, Jesus Owono mwenye umri wa miaka 20.
Kisha kulikuwa na ukaguzi wa VAR ili kuhakikisha kuwa Owono hakuwa ametoka mapena sana nje ya msitari wak kabla ya goli hilo kuthibitishwa na wachezaji wa Guinea ya Ikweta kuweza kukimbilia kundi la mashabiki wao uwanjani ili kusherehekea.
Michezo yote miwili iliisha 0-0 baada ya muda wa ziada na hatua ya 16 ilimalizika bila bao kutoka mchezo wa wazi.
Robo fainali ya kombe la Afrika sasa imepangwa, ambapo Burkina Faso itacheza dhidi ya Tunisia, Senegal itaumana na Guinea ya Ikweta, Gambia itakipiga dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo Cameroon.
Soma pia:Senegal na Morocco zatinga robo fainali AFCON
Misri, ambao wanashikilia rekodi ya ubingwa mara saba, watacheza na Morocco katika hatua hiyo ya nane bora mjini Yaounde siku ya Jumapili. Kikosi hicho cha Carlos Queiroz kimetinga robo-fainali licha ya kuwa wamefunga mara mbili pekee katika mechi zao nne nchini Cameroon kufikia sasa.
"Wakati mwingine penalti ni bahati nasibu na ni bahati nasibu, lakini leo nadhani timu bora uwanjani ilizawadiwa mikwaju ya penalti mwishoni, leo ilikuwa siku yetu," alisema Queiroz.
Huu ulikuwa mpambano wao wa 11 wa na bado Misri wamepoteza mara moja tu kwa Tembo -- miongoni mwa mafanikio yao mengi dhidi ya Ivory Coast ni ushindi wao wa mikwaju ya penalti katika fainali ya 2006.
"Siwezi kuwalaumu wachezaji. Sio kana kwamba walikosa kila penalti. Iliamuliwa kwa maelezo kidogo," kocha wa Ivory Coast Patrice Beaumelle alisema.
Soma pia: Misri na timu nyingine tano zatinga 16 bora ya AFCON
Mpangilio wa robo fainali ulikamilishwa na Guinea ya Ikweta, ambao waliishangaza Mali kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya sare ya 0-0 katika mchezo wa mwisho mjini Limbe.
Santiago Eneme alifunga mkwaju wa penalti muhimu kabla ya Mmali Falaye Sacko kupiga mkwaju uliookolewa na Jesus Owono, wakati nchi yake ikiondoka katika hatua ya kwanza ya mtoano kwa kombe la pili mfululizo la Mataifa ya Afrika.
Supastaa wa Liverpool, Salah alikuwa kivutio kikuu huko Douala, ambapo mashabiki walishangilia kila mara uso wake ulipoonekana kwenye skrini kubwa, lakini wakati mwingine alitatizika kwenye uwanja wa Japoma.
Mechi mbili zahamishwa kwenda Yaounde
Baada ya uvumi mwingi, Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, lilithibitisha kwamba mechi mbili za mwisho zilizopangwa kuchezwa uwanjani hapo zingehamishiwa Uwanja wa Ahmadou Ahidjo mjini Yaounde.
Rais wa CAF Patrice Motsepe alikuwa tayari amesema Jumanne kwamba mechi ya robo fainali itakayochezwa kwenye Uwanja wa Olembe mjini Yaounde pia itabadilishwa hadi Uwanja wa Ahmadou Ahidjo baada ya mkanyagano mkali uliosababisha vifo vya watu wanane.
Soma pia:Watu wanane wafariki katika mkanyagano AFCON
Hatua za nyongeza "hazihusiani na masuala ya usalama lakini zimechochewa na hali ya uwanja huko Japoma," afisa wa CAF aliliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
Robo fainali ya mwisho Jumapili, kati ya Senegal na Guinea ya Ikweta, na nusu fainali ya kwanza iliyopangwa Februari 2, ndizo mechi zinazohusika.
Uamuzi wa kuhamisha mechi nyingine ya robo fainali kutoka uwanja wa Olembe wenye viti 60,000 ulitangazwa rasmi siku ya Jumatano baada ya Motsepe kuandaa mkutano na waandaji wa michuano hiyo.
"Mechi inayofuata ambayo ilikuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Olembe haitafanyika hadi CAF na kamati ya maandalizi ya ndani watakapopata ripoti kamili ya kamati ya uchunguzi (ya tukio la Olembe) inayoonyesha mazingira na matukio yaliyosababisha majeraha na vifo vya watazamaji katika uwanja wa Olembe," CAF ilisema katika taarifa.
Nusu fainali ya pili, itakayochezwa Februari 3, na fainali ya Februari 6 bado zimepangwa kwenye uwanja wa Olembe kwa muda.
Soma pia: Mkuu wa CAF alaumu kufungwa lango katika mkasa wa AFCON
"Kamati ya CAF ya Maandalizi ya AFCON pia inahitaji uhakikisho kwamba hatua zinazofaa zimetekelezwa ili kuhakikisha kuwa tukio kama hilo halitatokea,” iliongeza taarifa hiyo.
Motsepe alisema Jumanne kwamba uamuzi "usioelezeka" wa kufunga lango la kuingilia ulihusika na tukio hilo ambalo lilisababisha vifo vya watu wanane na kujeruhi 38 kabla ya mechi kati ya wenyeji Cameroon na Comoro. Rais wa Cameroon Paul Biya pia ameamuru uchunguzi ufanyike.
Umati katika viwanja vyote ulikuwa umepunguzwa rasmi hadi asilimia 60 ya uwezo wa mashindano kwa sababu ya janga la corona, lakini kiwango cha juu kinapandishwa hadi asilimia 80 wakati Cameroon inacheza.
Uamuzi wa kuhamisha mechi kutoka Douala, wakati huo huo, ni pigo kwa mji huo mkuu wa kiuchumi wa taifa la Cameroon.
Uwanja huo ambao ulijengwa kwa ajili ya michuano hiyo na kugharimu dola milioni 230, utakuwa mwenyeji wa mchezo wake wa mwisho siku ya Jumamosi wakati Cameroon itakapocheza na Gambia.