1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal na Morocco zatinga robo fainali AFCON

26 Januari 2022

Senegal na Morocco zilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali kufuatia ushindi mtawalia dhidi ya Cape Verde na Malawi. Kuna wasiwasi hata hivyo juu ya hali ya nyota wa Senegal anaeichezea klabu ya Liverpool Sido Mani.

https://p.dw.com/p/464sG
Fußball Africa Cup of Nations | Senegal vs Kap Verde | Rote Karte
Picha: Gavin Barker/Sports Inc/empics/picture alliance

Sadio Mane aliamka baada ya mgongano mkali wa vichwa uliomuacha akiduwaa chini na yumkini kumsababishia jeraha la ubongo, na kufunga bao lililosaidia kuipeleka Senegal katika awamu inayofuata.

Senegal ilishinda 2-0 dhidi ya Cape Verde, ambayo iliwapoteza wachezaji wake wawili waliondolewa kwa kadi nyekundu, katika mechi iliyochezwa mji wa magharibi mwa Cameroon wa Bafoussam.

Soma pia: Cameroon yaizima Comoro AFCON, Gambia yatinga robo fainali

Nyota huyo wa Liverpool hakumaliza mechi na baadae alipelekwa hospitalini, ingawa alisema kwenye mtandao wa kijamii kwamba yuko sawa.

Fußball Africa Cup of Nations | Marokko vs Malawi
Achraf Hakimi wa Morocco akisherehekea goli lao la pili na wachezaji wenzie, katika uwnaja wa Ahmadou Ahidjo mjini Yaounde, Cameroon, Januari 25, 2022.Picha: MOHAMED ABD EL GHANY/REUTERS

Morocco iliifuata Senegal katika awamu ya nane bora kwa kutoka nyuma na kuishinda Malawi magoli 2-1. Kurudi kwa Morocco kulikamilishwa na mpira wa adhabu uliopigwa na mchezaji wa klabu ya Paris Saint-Germain, Achraf Hakimi, alieukunja mpiro juu ya ukuta na kuingia kwenye kona ya juu kwa goli la ushindi mnamo dakika ya 70.

Katika mechi ya Senegal dhidi ya Cape Verde, kadi nyekundu ya pili ya Cape Verde ilitolewa kwa mlinda mlango Vozinha, alipokimbia kutoka eneo lake kujaribu kuupiga mpira kichwa huku Mane akiufukuzia. Vichwa vya wachezaji hao viligongana vibaya, na Vozinha alipata mshtuko alipojaribu kuinuka baadae na kuishia kuyumbayumba.

Soma pia:Algeria yashindwa kulitetea taji lake AFCON

Vozinha aliodolewa kwa machela na hakuwepo kushuhudia kadi nyekundu iliyotolewa kwake na mwamuzi Lahlou Benbraham. Lakini maswali yataibuliwa juu ya kuruhusiwa kwa Mane kuendelea kucheza baada ya kuangukia uso kufuatia mgongano huo.

Mane alijikokota na kusimama kabla ya kufunga bao chini ya dakika 10 baadae katika dakika ya 63, wakati mpira wa kona ulipomdondokea mbali ya nguzo, na kupiga shuti la mguu wa kulia. Mshambuliaji huyo wa Liverpool hatimaye alibadilishwa katika dakika ya 70, akionekana dhahiri kuchechemea.

Afrika-Cup | Senegal - Guinea
Sadio Mane.Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Hiyo ilikuwa dakika 15 baada ya mgongano wa kichwa, ulioonekana mkali kutosha kumuondoa mara moja. Mane baadaye alichapisha kwenye ukurasa wa Facebook, picha yake na Vozinha wakiwa pamoja wakitabasamu hospitalini, ikiwa na maneno yasemayo: "Kila kitu ni kizuri."

Michuano hiyo ya kombe la mataifa ya Afrika iliendelea baada ya kutokea mgandamizo nje ya uwanja wakati wa mechi ya hatua ya 16 bora kati ya Cameroon na Comoro, na kusababisha vifo vya watu wanane na wengine saba wakiwa katika hali mbaya, hali iliyoyatia kiwingu mashindano ya juu ya soka barani Afrika.

Chanzo: AP