1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameroon yaizima Comoro AFCON, Gambia yatinga robo fainali

25 Januari 2022

Cameroon imehitimisha ndoto ya AFCON ya Comoro siku ya Jumatatu, lakini uchezaji wao thabiti umeamsha fahari kali katika taifa hilo la visiwani vya bahari ya Hindi. Gambia imeipiga kumbo Guinea kwa kuichapa goli 1-0.

https://p.dw.com/p/4624K
Fußball Africa Cup of Nations | Kamerun vs Komoren
Picha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP

Wenyeji wa michuano hiyo Cameroon wameweka miadi ya robo fainali dhidi ya Gambia, baada ya kupambana kushinda magoli 2-1 dhidi ya Comoro, ambao walilaazimika kuanza na mchezaji wa nje kama mlinda mlango huku wakicheza sehemu kubwa ya mechi hiyo ya jana wakiwa na wachezaji kumi.

Beki wa kushoto Chaker Alhadhur alianzia golini kwa Comoro mjini Yaounde, baada ya wawili kati ya walinda mlango wake watatu kuondolewa kutokana na maambukizi ya Covid-19, huku mwingine akikosekana kutokana na kuwa majeruhi.

Soma pia: Algeria yashindwa kulitetea taji lake AFCON

Kisha nahodha wao Nadjim Abdou alitolewa nje kwa kadi nyekundi dakika saba tu ndani ya mechi, na Karl Toko-Ekambi akaiweka Cameroon mbele kabla ya nahdodha Vincent Aboubakar kufunga bao lake la sita la mashindano.

Fußball Africa Cup of Nations | Kamerun vs Komoren
Nahodha wa Comoro Nadjim Abdou akioneshwa kadi nyekundu na kuondolewa mapema katika dakika ya 7. Licha ya kucheza punguzi, Comoro imeonesha mchezo wa hali ya juu.Picha: MOHAMED ABD EL GHANY/REUTERS

Licha ya hayo, ulikuwa uchezaji wa kishujaa kutoka kwa Wacomoro, ambao waliendeleza ndoto ya 16 bora hadi mwisho wa mechi, shukurani kwa mkwaju wa penati wa dakika za mwisho uliowekwa kimyani na Yousouf M'Changama.

Taifa hilo dogo la visiwa vya bahari ya Hindi lilifuzu kucheza awamu ya 16 bora katika mara yake ya kwanza kabisaa kushiriki michuano ya AFCON, baada ya kumaliza kama mmoja ya timu bora zilizoshika nafasi ya tatu katika awamu ya makundi.

Soma pia: Misri na timu nyingine tano zatinga 16 bora ya AFCON

Lakini ndoto yao iligeuka jinamizi baada ya jumla ya wachezaji wake 12 na wafanyakazi kukutwa na virusi vya corona siku mbili kabla ya mechi dhidi ya Cameroon, wakiwemo walinda mlango Ali Ahamada na Moyadh Ousseini.

Mlinda mlango mwengine, Salim Ben Boina, alijeruhiwa lakini walikuwa na matumaini kwamba Ahamada angeweza kuanza baada ya vipimo kuonesha hakuwa tena na maambukizi siku ya mechi. Lakini shirikisho la kandanda Afrika CAF, lilikataa kumruhusu kucheza kwa sababu vipimo vyake vya awali vilikuwa vimetoka siku mbili tu kabla.

Wachezaji hao, ambao kocha wao Amir Abdou alikuwa miongoni mwa waliokosekana baada ya kukutwa na virusi, walijikuta wakimkosa pia nahodha wao alietolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia uhakiki wa teknolojia ya VAR kuthibitisha kwamba alimfanyia madhambi Moumi Ngamaleu, lakini hawakukata tamaa.

Africa Cup of Nations - Gesamtansicht der kamerunischen Fans im Stadion
Mashabiki wa Cameroon wakitazama mechi ya duru ya 16 bora kati ya timu yao na Comoro, ambayo ilimalizika kwa ushindi wa 2-0, katika uwanja wa d'Olembe, Januari 24,01,2022.Picha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Hata hivyo ni Indomitable Lions wanaodumisha ndoto zao za kushinda Kombe la Mataifa katika ardhi ya nyumbani baada ya kufuzu kwa hatua ya nane bora ambapo watacheza mjini Douala dhidi ya Gambia siku ya Jumamosi.

Soma piaCameroon wafungua AFCON kwa ushindi:

Sawa na Comoro, timu ya Gambia iliyoorodheshwa katika nafasi ya 150 duniani inashiriki AFCON kwa mara ya kwanza lakini waliishangaza Guinea kwa kuilaza 1-0 katika mji wa magharibi wa Bafoussam mapema Jumatatu kutokana na bao kali la kipindi cha pili la Musa Barrow, anaeichezea klabu ya Bologna.

Mafanikio ya Gambia yalikuwa ya kushangaza zaidi baada ya kocha Tom Saintfiet kufichua kwamba kikosi hicho kiliathiriwa na sumu ya chakula wakati wa usiku. 

Hatua ya 16 bora itaendelea Jumanne hii ambapo Senegal itacheza na Cape Verde mjini Bafoussam kabla ya Morocco kumenyana na Malawi mjini Yaounde.