Miaka 100 ya Uturuki imefikia kusudio la Ataturk?
1 Novemba 2023Mustafa Kemal Ataturk alianzisha jamhuri ya Uturuki yenye mwelekeo wa sera za kimagharibi na kuanzisha mageuzi makubwa ambayo yalisitisha uongozi wa kiislamu "ukhalifa", lakini pia aliondoa matumizi ya maandishi ya Kiarabu kwa faida ya alfabeti ya Kirumi na kuwapa wanawake haki ya kupiga kura.
Uturuki, hata hivyo, imechukua muelekeo wa kihafidhina chini ya utawala wa miongo miwili wa rais Recep Tayyip Erdogan, ambaye chama chake kina mizizi katika vuguvugu za Kiislamu nchini humo na ambaye amekuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Uturuki tangu enzi za Ataturk.
Soma pia:Rais Erdogan asema magaidi hawatafaulu kufikia malengo yao baada ya mashambulizi ya Ankara
Miaka hii 100 ya Uturuki inampa Erdogan, ambaye alichaguliwa tena kwa muhula wa tatu mwezi Mei mwaka huu, nafasi ya kuunda mwelekeo na enzi mpya ya nchi hiyo ambayo aliitaja kuwa "Karne ya Uturuki."
Misingi ya kidini na mgawanyiko wa kitamaduni
Kumekuwa namgawanyiko wa kitamaduni wenye utata nchini Uturuki ukigubikwa na mjadala mkubwa kati ya wahafidhina na wale wanaoamini uwepo wa taifa huru lisiloegemea dini yoyote.
Kama mwanzilishi wa taifa hilo, Ataturk alidhamiria kuwa na nchi isiyo na misimamo ya kidini na kulifanya hilo kuwa sharti kuu la kisiasa.
Kwa miongo kadhaa, suala la kutenganisha uongozi na dini ilikuwa ni itikadi iliyokita mizizi nchini Uturuki.
Nchi hiyo iliweka marufuku ya kuvaa hijabu shuleni na katika taasisi za umma, ikaweka vikwazo kwa elimu za dini, kupitisha sera huria juu ya matumizi ya vilevi kama pombe, huku Msikiti wa Ufalme wa Ottoman" Hagia Sofia" ukigeuzwa kuwa jumba la makumbusho.
Soma pia:Azerbaijan yafanya luteka za kijeshi na Uturuki, karibu na Armenia
Lakini sera zote hizi zimewekwa kapuni chini ya utawala wa Erdogan, ambaye ameilekeza nchi katika misimamo ya kihafidhina.
Kwa sasa shughuli zote zilizo rasmi huanzishwa kwa maombi, huku mamlaka zinazoshughulikia masuala ya kidini zikipewa bajeti kubwa na idadi ya shule za kidini zikiongezeka.
Hata sera ya kiuchumi ya Erdogan ya kupunguza viwango vya riba na ambayo imesitishwa hivi karibuni, inadhaniwa ilichukuliwa kwa misingi ya kidini.
Soner Cagaptay, mtaalamu wa masuala ya Uturuki katika Taasisi ya Washington na mwandishi wa vitabu kadhaa kuhusu Erdogan, amesema Ataturk alikuwa mwanasiasa mwenye upeo mkubwa aliyeamini katika mfumo wa kijamii na alilenga kuifanya Uturuki kuwa ya kimagharibi zaidi na ambayo isiyoegemea dini yoyote.
Cagaptay ameongeza kuwa Erdogan anaamia pia katika mfumo wa Ataturk, lakini wanatofautiana kiitikadi.
Nafasi ya Uturuki katika diplomasia ya kimataifa
Uturuki yenye mwelekeo wa Magharibi ilijiunga na Jumuiya ya Kujihami NATO mnamo mwaka 1952 na kwa muda mrefu iliwasilisha maombi ya kujiunga na Umoja wa Ulaya, ingawa mazungumzo ya kuafiki au la uanachama huo yamesimama kwa sasa.
Kwa ujumla, maslahi ya Uturuki yaliendanana yale ya nchi za Magharibi katika sehemu kubwa ya Karne ya 20.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni, Uturuki imekuwa na uthubutu zaidi katika sera zake za kigeni na imekuwa ikilenga kupanua ushawishi wake wa kikanda na hata kimataifa.
Diplomasia hii mpya na iliyo huru inakuja na uwezekano wa kusababisha mgongano kati ya maslahi ya Uturuki na yale ya nchi za Magharibi.
Soma pia:Erdogan awasilisha ombi la Sweden kujiuna na NATO kwenye bunge la Uturuki
Hivi karibuni Uturuki imekuwa na mvutano na Umoja wa Ulaya kuhusu Syria, na Ankara imekuwa ikifanya mashambulizi ya kuvuka mpaka dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi PKK huko Syria na Irak, na pia ilizuia kwa muda uanachama wa Sweden kujiunga na NATO kwa madai kuwa Stockholm imekuwa ikiwahifadhi waasi hao.
Sera mpya ya mambo ya nje ya Uturuki imejikita pia kwenye uhusiano wake na mshirika wake mkuu wa biashara, Urusi.
Wakati nchi nyingi zaNATO zikichukua hatua kali dhidi ya Moscow kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine, Ankara imedumisha uhusiano wa karibu na Urusi ingawa inapinga vita hivyo na mara kadhaa imejaribu kuwa mpatanishi.
Cagaptay amesema malengo ya Ataturk na Erdogan ya kutaka kuifanya Uturuki kuwa taifa kubwa lenge nguvu na ushawishi yanashabihiana, lakini Ataturk aliamua kukumbatia na kunakili sera za kimagharibi za wakati huo.
Aliongeza kuwa, Erdogan kwa upande wake hana nia ya kuifanya Uturukikama kikaragosi cha sera za mataifa ya Ulaya, na anaamini kuwa anao uwezo wa kufanikisha lengo hilo pekee yake.