Erdogan alaani mashambulizi ya bomu katika jiji la Ankara
1 Oktoba 2023Erdogan ameyasema hayo kwenye hotuba yake kwa wabunge waliokutanika tena bungeni baada ya mapumziko ya majira ya joto.
Kwa mujibu wa shirika la Habari la serikali ya Uturuki Anadolu, Erdogan amesema wahusika hawakufikia malengo yao na kamwe hawatafanikiwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema mashambulio ya siku ya Jumapili yamewahusisha watu wawili.
Mshambuliaji wa kwanza alikufa baada ya kujitoa mhanga alitumia kifaa cha kulipuka katika eneo la katikati mwa mji mkuu wa Uturuki, Ankara, siku ya Jumapili.
Mwenzake aliuawa katika majibizano ya risasi kati yake na polisi.
Soma pia:Mshambuliaji ajitoa mhanga katikati mwa mji mkuu wa Uturuki
Jumuiya ya kujihami ya NATO ambayo Uturuki ni mwanachama imesisitiza kuwa inasimama pamoja na Uturuki katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amelaani shambulizi la Jumapili dhidi ya Wizara ya Mambo ya Ndani huko Ankara na amewatakia ahueni ya haraka maafisa wa polisi waliojeruhiwa.
Uturuki imefanya operesheni kadhaa kaskazini mwa Syria tangu mwaka 2016 kuwafukuza wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na wanamgambo wa Kikurdi, YPG, kutoka kwenye mpakani.
Uturuki inalichukulia kundi hilo la YPG kama washirika wa chama cha PKKkilichopigwa marufuku. Chama hicho cha PKK kimeorodheshwa kwenye makundi ya kigaidi na Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya. Wapiganaji wa PKK wanaendesha uasi dhidi ya Uturuki tangu mwaka 1984.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema serikali ya Uturuki itaendelea na mapambano dhidi ya magaidi, washirika wao, walanguzi wa madawa ya kulevya, na magenge ya uhalifu.
Hata hivyo waziri huyo wa Mambo ya Ndani hajasema mpaka sasa aliyehusikja na mashambulio ya Jumapili karibu na wizara yake na Bunge katika mji mkuu Ankara.
Vyanzo:DPA/AP/AFP