Mgombea upinzani ashinda urais jimbo la Lagos
27 Februari 2023gombea urais wa chama cha Labour, Peter Obi, ambaye kampeni yake iliwavutia vijana na wapigakura wengi wa mijini waliochoshwa na ufisadi, alishinda kura nyingi kwenye jimbo muhimu la Lagos, mji mkubwa kabisa barani Afrika.
Obi alitangazwa kupata kura 582,454 akimshinda kwa karibu sana gavana wa zamani wa jimbo hilo, Bola Tinubu, ambaye alipata kura 572,606 kutoka chama tawala APC, kwa mujibu wa matangazo ya Tume ya Uchaguzi (INEC), huku Atiku Abubakar wa chama kikuu cha upinzani, PDP, akipata kura 75,750.
Soma zaidi: Matokeo yaanza kutangazwa uchaguzi wa Nigeria
Awali Lagos ilikuwa ngome ya Tinubu, ambaye pia ndiye mgombea urais kutokea chama tawala.
Kampeni ya Obi kwa vijana
Obi alitumia kampeni yake kuwataka wapigakura kuvikataa vyama hivyo viwili ambavyo vimeitawala nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika kwa robo karne sasa, na ambavyo chini ya utawala wao ufisadi umetamalaki na ukosefu wa usalama umesambaa kote nchini humo.
Mgombea huyo wa chama cha Labour alikuwa mashuhuri sana miongoni mwa vijana, hasa wa mijini, ambao wana kiwango kikubwa zaidi cha elimu na wenye fursa ya kutumia simu za mikononi na mitandao ya kijamii, lakini bado anakabiliwa na kibarua kigumu kwenye maeneo ya vijijini yenye wapigakura wahafidhina.
Kasi ndogo ya kuhesabu na kutangaza matokeo imekosolewa na vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo, ambavyo vinaikosoa Tume ya Uchaguzi kwa matayarisho dhaifu.
Uchaguzi wa amani
Takribani, watu milioni 90 waliandikishwa kupiga kura kwenye uchaguzi wa jana, Jumapili, kumpata mrithi wa Rais Muhammadu Buhari, wengi wakitarajia kiongozi wao mpya atayatatuwa matatizo ya ukosefu wa usalama, hali mbaya ya kiuchumi na kuenea kwa umasikini.
Kwa sehemu kubwa, upigaji ulikwenda salama, ukiacha matukio machache ya washambuliaji waliovamia vituo vya kupigia kura, huku vituo vingi vikibakia wazi muda mrefu jijini Lagos na miji mingine.
Wapigakura wengi waliripotiwa kubakia vituoni usiku mzima kusimamia uhisabuji kura.
Soma zaidi: Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Nigeria
Nigeria yapiga kura kuchagua rais na bunge
Pamoja na kuibuka kwa chama kidogo cha Labour, bado kwa kiasi kikubwa, uchaguzi huu ni kinyang'anyiro baina ya gavana wa zamani wa Lagos, Bola Tinubu mwenye umri wa miaka 70, wa chama tawala cha APC, na makamu rais wa zamani, Atiku Abubakar, mwenye umri wa miaka 76, kutoka chama cha upinzani cha PDP.
Tume ya Uchaguzi ya Nigeria ilianza kutangaza matokeo ya jimbo kwa jimbo kwa uchaguzi huo mkuu wa Jumamosi, lakini haifahamiki ikiwa itaweza kumtangaza mshindi rasmi wa uchaguzi ndani ya siku chache zijazo.