1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yapiga kura kuchagua rais na bunge

25 Februari 2023

Mamilioni ya raia wa Nigeria wamepiga kura kumchagua rais mpya na Bunge jipya la taifa hilo lililo na idadi kubwa ya watu barani Afrika, na lilnalopitia kipindi kigumu cha ukosefu wa fedha

https://p.dw.com/p/4NyjG
Nigeria | Wahltag
Picha: Uwais Abubakar Idris/DW

Wakiwa na shauku ya mabadiliko baada ya miaka kumi ya rais Muhamadu Buhari, mamia kwa maelfu ya raia wa taifa hilo wameteremka vituoni kupiga kura tangu mapema asubuhi kuamua nani atakuwa kiongozi ajaye.

Wagombea wakuu watatu ndiyo wanawania kiti cha rais kumrithi Buhari anayehitimisha kipindi chake cha pili.

Bola Tinubu,  anawania kupitia chama tawala APC huku Atiku Abubakar akipepereusha bendera ya chama kikuu cha upinzani cha PDP.Mgombea mwengine wa tatu ni  Peter Obi wa chama cha Labour anaeungwa mkono na idadi kubwa ya wapiga kura vijana nchini humo.

Tume huru ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema haifahamu hasa ni wakati gani matokeo yatakuwa tayari lakini wameahidi kulifanya zoezi la kuhesabu kura kwa haraka.