Meli kutoka Ukraine kutia nanga Istanbul baadae leo
2 Agosti 2022Meli hiyo ya mizigo inayoitwa Razoni ilisafiri katika pwani ya Romania usiku kucha. Mamlaka ya usafiri wa majini ya Marine Traffic,ilitangaza kuwa hapo awali meli hiyo ilikuwa imesonga pole pole sana katika maji ya Ukraine kutokana na uwezekano wa mabomu yaliotegwa kwenye eneo hilo,lakini ilishika kasi baadaye usiku.
Umoja wa Mataifa umesema meli hiyo imebeba zaidi ya tani 26,000 za ngano. Kwenye bandari ya Instabul, itakaguliwa na kituo maalum cha uratibu wa pamoja kilichoanzishwa Jumatano iliyopita na chenye wafanyikazi ambao ni maafisa wa kiraia na kijeshi kutoka Ukraine na Urusi, pamoja na wajumbe kutoka Uturuki na Umoja wa Mataifa.
Ukraine na Urusi ndizo zilizokuwa wasambazaji wakubwa wa chakula hicho muhimu duniani kabla ya Urusi kuivamia Ukraine mwezi Februari. Bidhaa kutoka Ukraine zilianza kutokupatikana kwa sababu Urusi inaidhibiti Bahari Nyeusi. Kwenye mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimhakikishia kuendelea kwa juhudi za Ulaya kusaidia Kyiv kuuza nje nafaka zake.
Soma pia→Meli ya kwanza yenye nafaka za Ukraine yaondoka Odesa
''Urusi mara kwa mara ilichochea njaa katika nchi za Afrika na Asia''
Kulingana na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kouleba, meli zingine 16 zilizojaa nafaka zinasubiri zamu yao kuondoka bandari ya Odessa, ambayo kabla ya vita bandari hiyo ilidhibiti asilimia sitini ya shughuli za kibiashara nchini humo.
Hata hivyo rais Zelensky alisema ni mapema mno kutabiri hatua zitakazofuata. Amesema ni vyema kusubiri kuona jinsi mkataba utakavyofanya kazi na ikiwa usalama utahakikishwa.
''Hatuwezi kuwa na dhana potofu kwamba Urusi itajiepusha tu na kujaribu kuvuruga mauzo ya nje ya Ukraine. Urusi mara kwa mara ilichochea njaa katika nchi za Afrika na Asia, ambazo kimsingi zimeagiza kutoka nje kiasi kikubwa cha chakula cha Ukraine.''
Na kuongeza : ''Na sasa katika hali ya joto kali, kama mwaka huu barani Ulaya, tishio la mgogoro wa bei na uhaba fulani wa chakula pia inawezekana kwa baadhi ya nchi za Ulaya.'', alisema Zelensky.
Soma pia→ Urusi yasema mashambulizi bandari ya Odessa yalilenga silaha za Marakeni
EU yapongeza hatua ya mwanzo
Kwa upande wake, Uturuki inataraji kuondoka kwa meli za nafaka kutoka Ukraine angalau kila siku. Zaidi ya tani milioni 20 za ngano kutoka mavuno ya mwaka jana bado zinasubiri kusafirishwa, kwa mujibu wa Ukraine. Umoja wa Ulaya umepongeza hatua hiyo ya kusafirishwa shehena ya ngano kutoka Ukraine, lakini umesema ni ya kwanza tu kuelekea kupunguza makali ya mzozo wa chakula duniani.