1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi bandari ya Odessa yalilenga silaha za Marakeni

24 Julai 2022

Wizara ya ulinzi ya Urusi inasema mashambulizi dhidi ya bandari ya Odessa yalilenga silaha zilizotumwa na mataifa ya Magharibi na hayavunji makubaliano yaliyofikiwa kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul.

https://p.dw.com/p/4EZcS
Ukraine-Krieg Odesa |  Raketenangriff auf Hafen
Picha: Efrem Lukatsky/Odesa City Hall/AP/picture alliance

Msemaji wa wizara hiyo ya ulinzi, Igor Konashenkov, alisema siku ya Jumapili (Julai 24) kwamba kilichoshambuliwa kwenye bandari ya Odessa ni "meli ya kivita ya Ukraine na ghala la silaha lenye makombora aina ya Harpoon ya kushambulia meli za kijeshi ambayo yameletwa na Marekani."

Mashambulizi hayo ya Urusi yalifanyika siku moja tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano yaliyosimamiwa na Uturuki kuruhusu usafirishaji wa ngano na bidhaa nyengine za kilimo kutoka bandari ya Odessa kwenda mataifa mengine duniani siku ya Ijumaa (Julai 22).

Mapema Rais Volodymyr Zelensky alisema kwenye hotuba yake ya kila usiku siku ya Jumamosi (Julai 23) kwamba mashambulizi hayo ya Odessa "yalivunja kila uwezekano wa majadiliano na Urusi."

Jeshi la Ukraine lilisema jioni ya Jumamosi kwamba Moscow ilikuwa imeishambulia bandari hiyo kwa makombora manne kutoka melini, mawili kati yake yakadunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine.

'Hakuna ghala la ngano lililoshambuliwa'

Ukraine-Krieg Odesa | Raketenangriff auf Hafen
Wazima moto wakijaribu kuokowa kilichosalia kwenye eneo lililoshambuliwa na kombora la Urusi katika bandari ya Odessa siku ya Jumamosi (Juli 22, 2022).Picha: UKRAINIAN ARMED FORCES/REUTERS

Msemaji wa kamandi ya kijeshi, Nataliya Humenyuk, alisema kwamba hakuna ghala hata moja la silaha lililopigwa. 

Hata hivyo, waziri wa ulinzi wa Uturuki alisema alikuwa na taarifa kutoka mamlaka za Ukraine kwamba kombora moja lilipiga ghala la ngano huku jengine likianguka karibu yake, ingawa hakuna lilioathiri upakiaji kwenye bandari hiyo.

Haikufahamika mara moja ni kwa namna gani mashambulizi hayo yangeliathiri mipango ya kuanza tena kwa usafirishaji wa ngano ya Ukraine kupitia njia salama katika bandari tatu za Bahari Nyeusi: Odessa, Chernomorsk na Yuzhny.

Siku ya Ijumaa (Julai 22), Urusi na Ukrainezilisaini mikataba miwili na Umoja wa Mataifa na Uturuki mjini Istanbul iliyodhamiriwa kusafisha njia kwa ajili ya usafirishaji wa mamilioni ya tani za ngano inayohitajika sana ulimwenguni na pia usafirishaji wa ngano na mbolea ya Urusi.

Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa walielezea matumaini yao kwamba makubaliano hayo yangelimaliza miezi kadhaa ya mkwamo ambao ulisababishwa na vita nchini Ukraine na ambao ulitishia kuiingiza dunia nzima kwenye janga la njaa.

Mikataba hiyo inazitaka pande zote mbili - Urusi na Ukraine - kujiepusha na kurusha makombora kwenye bandari za Bahari Nyeusi.