Meli ya kwanza yenye nafaka za Ukraine yaondoka Odesa
1 Agosti 2022Meli hiyo imeondoka tangu yalipofikiwa makubaliano kati ya Ukraine na Urusi ya kuumaliza mzozo wa chakula duniani kutokana na Urusi kuivamia Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari.
Waziri wa Uchukuzi wa Ukraine, Oleksandr Kubrakov, amesema kuwa meli hiyo ya mizigo inayoitwa Razoni na yenye bendera ya Sierra Leone, ilikuwa imebeba zaidi ya tani 26,000 za mahindi.
Makubaliano yalifikiwa Julai
Julai 22, Urusi na Ukraine zilisaini makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, yenye lengo la kuona kuwa nafaka inasafirishwa kutoka kwenye bandari tatu za Ukraine zilizoko katika Bahari Nyeusi. Kubrakov amesema nchi yake imeanza hatua muhimu za mwanzo za kusafirisha nafaka hiyo.
''Upande wa Ukraine tumeanza kuchukua hatua zote muhimu kwa ajili ya kuanza kusafirisha nafaka yetu kwa njia ya bahari, kutoka kwenye bandari zetu. Bandari zetu mbili ziko tayari kuanza, ni za Chornomorsk na Odesa. Tuna matumaini ya kuiandaa pia bandari ya Pivdennyi,'' alifafafaanua Kubrakov.
Ukraine imesema misafara mingine itakayokuwa na shehena ya nafaka inatarajiwa kufuata kwa kuzingatia na kuheshimu ukanda wa bahari na taratibu nyingine zinazoendana na makubaliano hayo. Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imesema katika taarifa yake leo kuwa meli hiyo inatarajiwa kufika Istanbul Jumanne na itaendelea na safari bada ya kukaguliwa mjini humo.
Kwa mujibu wa Ukraine, zaidi ya tani milioni 20 za nafaka zilizovunwa mwaka jana, bado zinasubiri kusafirishwa nje ya nchi hiyo. Ikulu ya Urusi imesema leo kuwa hatua ya meli ya nafaka kuondoka katika bandari ya Odesa ni ishara nzuri. Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kubela aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba ''leo ni siku ya ahueni kwa ulimwengu na hasa kwa watu wa Mashariki ya Kati, Asia na Afrika''.
Umoja wa Mataifa wapongeza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameipongeza hatua ya kuondoka kwa meli hiyo. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Guterres ana matumaini kwamba misafara mingine itafuata na kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na kwamba huo utakuwa mwanzo wa meli nyingine nyingi za biashara kufanya safari zake kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa. Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema hatua hiyo italeta utulivu na unafuu unaohitajika kwa usalama wa chakula duniani.
Ama kwa upande mwingine Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu ICRC, imesema haijapewa ruhusa ya kulitembelea gereza la Olenivka, ambako wafungwa wa kivita wa Ukraine walikufa katika shambulizi lililotokea kwenye gereza hilo.
Wakati huo huo, shambulizi la Urusi katika jimbo la Mykolaiv, limemuua Oleksiy Vadatursky, mwanzilishi wa biashara kubwa ya kilimo nchini Ukraine. Gavana wa jimbo la Mykolaiv, Vitaliy Kim amesema kuwa tajiri huyo aliuawa Jumapili pamoja na mkewe.
Aidha, taarifa zilizotolewa na Gavana wa Donetsk, Pavlo Kyrylenko zinaeleza kuwa raia watatu wameuawa na shambulizi la Urusi lililotokea kwenye jimbo hilo, huku wawili wakiuawa kwenye mkoa wa Bakhmut na mmoja karibu na mji wa Soledar, ndani ya muda wa saa 24.
(AP, DPA, AFP, Reuters)