1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky ashuhudia upakiaji wa nafaka Odesa

29 Julai 2022

Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky ameitembelea bandari ya Bahari Nyeusi kuonyesha kuwa nchi yake iko tayari kuanza kusafirisha nafaka chini ya mpango uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/4EsL0
Videostil Wolodymyr Selenskyj
Picha: APTN

Akiwa kwenye ziara ya nadra nje ya mji mkuu Kyiv tangu uvamizi wa Urusi wa Februari 24, Rais Zelensky amekemea mzingiro wa Urusi wa Bahari Nyeusi ambao umeizuia Ukraine kusafirisha nafaka, hali inayochangia kupanda pakubwa kwa bei za nafaka ulimwenguni. Rais huyo wa Ukraine amesema wakati akiwa katika bandari ya Chornomorsk karibu na mji wa kusini wa Odesa kuwa anatumai usafirishaji wa nafaka utaanza leo au kesho. Hii ni meli ya kwanza inayopakiwa tangu vita vilipoanza. Hapa nimesimama mbele ya meli ya Uturuki. Ina maana bandari imeanza kufanya kazi. Kitu muhimu zaidi kwetu ni kuwa bandari inafanya kazi, watu wanafanya kazi.

Getreide-Terminal in Odessa Region
Bandari za Ukraine zilifungwa tangu FebruariPicha: picture alliance/NurPhoto

Soma pia:Ukraine yaanza tena shughulli za ugavi wa nafaka katika bandari

Hata hivyo amesema usafirishwaji wa ngano na nafaka nyingine utaanza na meli kadhaa ambazo zilikuwa tayari zimepakiwa lakini hazingeweza kuondoka bandari za Ukraine.

Ukraine ni muuzaji mkubwa ulimwenguni wa ngano, shayiri, mahindi na mafuta ya alizeti na kupotea kwa bidhaa hiyo kumepandisha bei za chakula ulimwenguni, kutishia ukosefu wa usalama wa kisiasa na kusaidia kuwasukuma watu Zaidi katika umaskini na njaa katika nchi ambazo tayari ziko hatarini. Zelensky amesema jeshi la Ukraine limedhamiria kuhakikisha usalama wa meli, akiongeza kuwa ni muhimu kuwa Ukraine iwe nchi inayohakikisha upatikanaji wa chakula ulimwenguni.

Soma pia: Urusi yatoa hakikisho la usafirishaji wa ngano

Ukraine, Urusi na Umoja wa Mataifa zilikubaliana wiki iliyopita kuwezesha usafirishaji wa ngano na nafaka nyingine kutoka bandari za Ukraine kupitia maeneo salama kwenye Bahari Nyeusi, Pamoja na mbolea na chakula kutoka Urusi.

Ukraine-Krieg | Abkommen über Export von ukrainischem Getreide
Umoja wa Mataifa unasimamia usafirishaji nafakaPicha: OZAN KOSE/AFP

Msemaji wa Kremlin Dimtry Peskov amesisitiza leo umuhimu wa kudumisha uhusiano kati ya kusafirisha nafaka kutoka bandari za Ukraine na kuondoa vizuizi vya moja kwa moja au visivyo vya moja kwa moja vya usafirishaji wa nafaka, mbolea na bidhaa nyingine kwa masoko ya kimataifa.

Wasiwasi wa usalama na ugumu wa makubaliano yaliyofikiwa vimefanya shughuli hiyo kuchelewa kuanza ambapo mpaka sasa hakuna nafaka zozote zilizoondoka bandari za Ukraine. Kipa upande unakabiliwa na changamoto ya muda unaoyoyoma kwa sababu muafaka huo unadumu tu kwa siku 120.

Lengo katika miezi minne ijayo ni kusafirisha karibu tani milioni 20 za nafaka kutoka bandari za Ukraine zilizozingirwa tangu uvamizi wa Februari 24. Hiyo inatoa muda wa karibu meli nne hadi tano kubwa kwa siku kusafirisha nafaka kutoka bandari hizo kuwapelekea mamilioni ya watu Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, ambayo tayari wanakabiliwa na uhaba wa chakula na katika baadhi ya maeneo, njaa.

Ukrainisches Getreide soll wieder auf den Weltmarkt kommen
Ukraine ni muuzaji mkubwa wa nafaka ulimwenguniPicha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Waziri wa miundombinu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov, amewaambia waandishi Habari katika bandari ya Odesa leo kuwa Ukraine iko tayari na sasa inasubiri tu Umoja wa Mataifa kuthibitisha maeneo salama ambayo yatatumiwa na meli zinazopita baharini.

Muafaka huo unasema kuwa Urusi na Ukraine zitoe uhakikisho wa kiwango cha juu kwa meli zinazopita katika Bahari Nyeusi kwenda bandari tatu za Ukraine: Osdesa, Chernomorsk na Yuzhny. Meli hizo zitaongozwa na boti ndogo kupitia maeneo salama yaliyoidhinishwa. Operesheni nzima itasimamiwa na Kituo cha Pamoja cha Uratibu mjini Istanbul chenye maafisa kutoka Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa.

Mara baada ya meli kufika bandarini, zitapakiwa na maelfu ya tani za nafaka kabla ya kuelekea katika mlango wa bahari wa Bosphorus, ambako zitafanyiwa ukaguzi kuona kama kuna silaha. Kutakuwa na ukaguzti kwa meli zinazoelekea Ukraine pia.

ap, afp, dpa, reuters