Mazungumzo ya kujadili vita vya Gaza kufanyika Saudi Arabia
26 Aprili 2024Wanadiplomasia wakuu wa nchi za Kiarabu na Ulaya wanatarajiwa kuanza kuwasili katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, mwishoni mwa wiki hii kushiriki mkutano wa kilele wa kiuchumi pamoja na mikutano kuhusu vita huko Gaza.
Mkutano huo maalum wa siku mbili wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia, umepangwa kuanza siku ya Jumapili, na utawajumuisha miongoni mwa viongozi wengine, mawaziri wa mambo ya nje wa Saudia, Jordan, Misri na Uturuki.
Soma zaidi:Mataifa ya kiisalam yaikosoa Marekani katika vita ya Gaza
Siku ya Jumatatu, kutafanyika kikao kitakachoangazia vita vya Gaza na kinatarajiwa kumshirikisha Waziri Mkuu mteule wa Palestina Mohammed Mustafa, Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly na Sigrid Kaag, mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa huko Gaza. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Stephane Sejourné ni miongoni mwa maafisa wa Ulaya watakaosafiri kuelekea Saudi Arabia kuhudhuria mkutano huo.
Misri yatuma ujumbe huko Israel
Ujumbe huo wa ngazi ya juu kutoka Misri na unaoongozwa na afisa mkuu wa upelelezi wa Misri, Abbas Kamel, unalenga kujadili na Israel kuhusu mipango ya usitishwaji mapigano kwa muda mrefu huko Gaza. Wakati huo huo, serikali mjini Cairo imeonya kuwa mashambulizi ya Israel katika mji wa Rafah unaopakana na Misri, yatakuwa na athari kubwa kwa utulivu wa kikanda.
Wakati vita vikiendelea kupamba moto huku idadi ya vifo na majeruhi vikiongezeka, shinikizo la kimataifa pia limeongezeka la kuzitaka Israel na kundi la Hamas wafikie makubaliano ya kusitisha mapigano.
Raia wa Jordan waliandamana leo baada ya sala ya Ijumaa kuwaunga mkono Wapalestina. Qassem Al-Kubaai ni mmoja wao:
"Baada ya siku 200 za mashambulizi, baada ya mashahidi elfu 34,000 kuuawa, baada ya laki moja ya wengine kujeruhiwa na kusalia chini ya vifusi, baada ya kubomolewa kwa shule na hospitali, na baada ya yote hayo, ni wakati sasa wa serikali na nchi za Kiarabu kuchukua hatua."
Soma pia: Viongozi wa mataifa ya kiarabu na kiislamu wataka kukomeshwa vita vya Gaza
Afisa wa Misri amesema kwa sharti la kutotajwa jina kuwa mazungumzo ya leo huko Tel-Aviv yatalenga kwanza juu ya ubadilishanaji wa mateka wanaoshikiliwa na Hamas pamoja na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel. Kutajadiliwa pia suala la kurejeshwa kwa idadi kubwa ya Wapalestina waliokimbia makazi yao kaskazini mwa Gaza.
(Vyanzo: Mashirika)