1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya kiarabu na kiislamu yataka kukomeshwa vita Gaza

11 Novemba 2023

Viongozi wa mataifa ya kiarabu na yale ya Kiislamu wametoa mwito leo wa kusitishwa haraka operesheni zote za kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza na kuitwika dhima Israel ya kile wamekitaja kuwa "uhalifu" dhidi ya Wapalestina.

https://p.dw.com/p/4YhSo
Mkutano wa mataifa ya kiarabu na yale ya Kiislamu mjini Riyadh
Viongozi wa mataifa ya kiarabu na yale ya Kiislamu kwenye mkutano wa mjini RiyadhPicha: WANA NEWS AGENCY/REUTERS

Mwito huo umetolewa wakati wa mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na zile za Kiislamu uliofanyika leo nchini Saudi Arabia, kwa malengo ya kutoa shinikizo kwa Israel kuachana na kampeni yake ya kijeshi huko Ukanda wa Gaza.

Kwenye hotuba yake mwenyeji wa mkutano huo, Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman amesema nchi hiyo inalaani kile amekiita "vita vya kikatili" dhidi ya ndugu zao Wapalestina. Matamshi sawa na hayo yametolewa na viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ikiwemo wale wa mataifa ya Uturuki, Qatar, Misri na Syria.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amekwenda mbali zaidi na kuwataka viongozi wenzake kuiwekea vikwazo Israel ikiwa ni pamoja na kuinyima mafuta na kususia kununua bidhaa za nchi hiyo.