Mataifa tajiri yahodhi mamilioni ya chanjo za Mpox
12 Septemba 2024Hii ni kulingana na takwimu za shirika la habari la Reuters, nyaraka na makadirio kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali. Lakini swali ni je, nchi hizo ziko tayari kuzigawanya?
Chanjo hizo zimehifadhiwa kwa miaka kadhaa na nchi kama Japan, Marekani na Canada kutumika iwapo kutazuka tena mripuko wa ugonjwa wa ndui ambao ni hatari zaidi.
Baadhi ya chanjo hizo zilitumiwa nje ya Afrika mnamo mwaka 2022 wakati mpox ilipoenea kote ulimwenguni.
Waatalamu wa magonjwa wanasema sehemu ndogo ya dozi hizo inaweza kusaidia kupunguza kile kinachoonekana sasa kuwa mlipuko mkubwa zaidi wa mpox katika historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi jirani.
Kupitia taarifa, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika -CDC- kimesema chini ya dozi milioni 4 zimeahidiwa kutolewa kama msaada kwa kiasi kinachokadiriwa cha kati ya milioni 18 na 22 zinazohitajika kuwapa chanjo watu milioni 10 katika muda wa miezi sita kulingana na chanjo.
Soma pia:Kongo yapokea chanjo zaidi za ugonjwa wa Mpox kutoka Marekani
Maria Van Kerkhove, kaimu mkuu wa kitengo cha kuzuia majanga katika Shirika la Afya Duniani WHO, ameiambia Reuters kwamba anapigia upatu michango zaidi pamoja na CDC na mashirika mengine ya afya.
Wataalamu wa magonjwa wanasema chanjo za Mpox peke yake hazitoshi na nchi zilizoathirika pia zinahitaji kuweza kupima magonjwa na kufanya uhamasishaji kukabiliana na miripuko ipasavyo.
Lakini mgawanyiko mkubwa wa upatikanaji wa chanjo unaonyesha kuwa serikali bado hazijajiandaa kukabiliana na vitisho vya miripuko ya virusi pale inapoanza na kabla ya kuenea.
Chanjo zinazopendekezwa na WHO zimehifadhiwa duniani.
Jynneos ya Bavaria Nordic, KM Biologics' LC16; na ACAM2000. Chanjo hizo zote zinazingatiwa kwa ununuzi na msaada barani Afrika, kulingana na msemaji wa Gavi, kundi la kimataifa linalosaidia nchi za kipato cha chini kununua chanjo. Kundi hilo lina hadi dola $500 milioni za kusaidia kukabiliana na mpox.
Nchi nyingi tajiri zinakataa kuelezea kiasi cha chanjo zilizonazo zikitoa sababu za usalama wa taifa. Japan ina takriban dozi milioni 200 za LC16, kutoka mwaka 2022. Hii ni kulingana na WHO.
Kacita, amesema Kongo iko kwenye majadiliano ya hadi dozi milioni 3.5 za LC16 kutoka Japan. KM Biologics ilikataa kutoa maoni.
Soma pia:Shehena ya kwanza ya chanjo za Mpox kuwasili Kongo Alhamisi
Afisa wa afya wa Japan amesema Kongo iliomba dozi milioni 3.05, lakini hakuthibitisha muda wa utoaji. Amesema takwimu ya dozi milioni 200 ya WHO haikuwa sahihi lakini hakuthibitisha kiasi cha hifadhi ya taifa.
Adam Houston, mshauri wa matibabu wa shirika la Medecins Sans Frontiere, Canada, anasema huenda nchi hiyo ina hadi dozi milioni 2 kutoka Bavarian Nordic katika hifadhi yake, kulingana na matangazo ya awali kutoka kwa kampuni hiyo. Dozi hizo zilitumiwa kukabiliana na mripuko wa mpox wa mwaka 2022 nje ya Afrika. Wiki hii, serikali ya Canada imesema itachangia hadi dozi 200,000.
Marekani haijaweka wazi akiba yake
Maafisa wa Marekani wamekataa kufichua kiasi cha chanjo kilichoko katika hifadhi yake lakini maafisa wawili wakuu wa utawala katika serikali ya Rais Joe Biden, wamesema dozi hizo zinatosha kuwalinda watu wake.
Uhispania ni miongoni mwa wafadhili wakubwa waliothibitishwa, ikiahidi mwezi Agosti asilimia 20 ya hifadhi yake ya chanjo ya mpox, au dozi 500,000. Nchi hiyo imezitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya kufanya hivyo.
Soma pia:Ufadhili wa mapambano ya Mpox Afrika wachechemea
Halmashauri ya Ulaya ina mkataba wa pamoja wa ununuzi na Bavarian Nordic kununua chanjo za msaada na imetuma dozi 215,000 kwa Kongo.
Msemaji wa timu ya Afrika CDC nchini Kongo, anasema baadhi ya chanjo zinaweza kugharimu takriban dola 150 kwa mtu mmoja kupata chanjo kamili, bei ambayo wengi hawawezi kumudu katika nchi za Afrika, hivyo basi chanjo za msaada kutoka kwa nchi nyingine ni muhimu zaidi.