1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya haki za binadamu yataka majadiliano Tanzania

George Njogopa28 Julai 2021

Mashirika ya kutetea haki za binadamu Tanzania yametoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na viongozi wa upinzani ili kutatua masuala yanayozusha msuguano kufuatia kukamatwa wenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

https://p.dw.com/p/3yCbZ
Tansania Pressekonferenz zu Übegriffen auf Journalisten
Picha: DW/S. Khamis

Mashirika hayo yanaona kwamba upepo wa kisiasa unavyoanza kubadilika wakati huu, siyo ishara njema kwa mustakabali wa taifa ambalo lilianza kuonyesha nia ya maridhiano tangu kuanza kwa utawala wa awamu ya sita.

Na Rais Samia mwenyewe katika hotuba yake ya kwanza Bungeni, alidokeza kiu yake ya kutaka kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani kwa ajili ya kuangalia njia bora ya kuendesha shughuli za kisiasa ingawa hadi sasa bado hajafanya hivyo, lakini tayari amekutana na makundi kama ya wazee, wanawake na vijana.

Soma pia: Tanzania : upinzani waapa kuendelea kudai mabadiliko ya katiba

Wito wa mashirika ya haki za binadamu unakuja kufuatiwa kutiwa nguvuni kwa mwenyekiti wa chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa akiongoza makongamano ya ndani yenye shahaba ya kuamusha vuguvugu la madai ya katiba mpya. Mwanasiasa huyo hivi sasa yuko gerezani baada ya kushtakiwa kwa makossa ya ugaidi.

Tansania Oppositionspolitiker Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ameshtakiwa kwa makosa ya ugaidi Tanzania.Picha: DW/S. Khamis

Haja ya kukaa na kuzungumza

Katika rai, yake, mratibu mkuu wa mtandao wa haki za binadamu, Onesmo Ole Ngrumwa anasema ni vyema kukawa na meza ya majadiliano kwa pande zote ili kuzuwia hali ya sintofahamu inayoweza kujitokeza katika siku za usoni.

Katika wiki za hivi karibuni, Chadema imekuwa ikiendesha makongamano ya ndani katika maeneo mbalimbali ya nchi, makongamano ambayo hujadili haja ya Tanzania kuwa na katiba mpya.

Kongamano lake la Mwanza lilishindwa kufanyika baada ya askari polisi kumtia mbaroni Mwenyekiti Mbowe ambaye  ndiye alitarajiwa kuwa mzungumzaji mkuu.

Soma pia: Chadema kuendelea na makongamano ya Katiba mpya

Kuhusu wananchi kuendesha makongamano pamoja na uhuru wa maoni, rais wa chama cha wanasheria cha Tanginyika Law Society, Dr Edward Hoseah katika mahojiano yake aliyofanya jana na kituo kimoja cha televisheni alisema ni utamaduni mbaya kubana uhuru ulioruhusiwa kisheria.

Wapinzani kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisema, licha ya kadhia iliyomkumba mwenyekiti Mbowe, bado wanaamini vuguvugu la kutaka mabadiliko ya katiba mpya lingali hai na wameahidi kuendelea nalo.