Miito yahanikiza Tanzania kumuachia Freeman Mbowe
26 Julai 2021Jeshi la polisi hadi sasa halijatoa taarifa yoyote wala kutoa tamko lingine kuhusu sakata hilo mbali na taarifa yake ya mwisho iliyoonesha kwamba, Mbowe aliletwa Dar es Salaam akitokea Mwanza na anatuhumiwa kwa makosa ya ugaidi makosa ambayo yanafanya makundi ya watu kugawika kimaoni kutokana na tuhuma hizo.
Katika ujumbe wake aliotuma kwa wanachama wake kupitia kwa familia yake, Mbowe amesema licha ya yale anayopitia bado hatavunjika moyo na juhudi zake za kisiasa.
James Mbowe ambaye ni mmoja wa wanafamilia wake, amesema Mbowe ameonekana kuwatia moyo wale wanaoendesha vuguvugu la kudai katiba mpya kutorudi nyuma.
Chama chake Chadema kimelaani hatua ya kuendelea kushikiliwa kwa kiongozi huyo na kulingana na mkurugenzi wa itifaki ya mambo ya nje wa chama hicho, John Mrema ameimbia DW kuwa Mbowe anajisikia vibaya kiafya.
Mbowe aliletwa jijini Dar es salam mwishoni mwa wiki akiwa na viongozi wengine kadhaa waliokamatwa jijini Mwanza, lakini viongozi hao wengine wameachiwa wakati yeye akiendelea kushikiliwa na jeshi hilo.
Chama cha wanasheria chaungana na wanaotoa miito ya kuachiwa Mbowe
Tangu kukamatwa kwake kwa tuhuma zinazomkabili, kumekuwa na miito inayoendelea kutolewa ikitaka kuachiwa kwake huru au afikishwe mahakamani.
Miongoni mwa walijitokeza kuzungumzia sakata hilo, ni pamoja na chama cha wanasheria cha Tanganyika Law Society kilicholaani tukio hilo, kikisema limefanywa kinyume na katiba ya nchi.
Rais wa chama hicho Dokta Edward Hoseah katika ujumbe wake aliotuma kwa njia ya mtandao wa kijamii amesema msimamo kamili wa TLS utatolewa baada ya baraza la uongozi kukutana na kujadili jambo hilo.
Wakati hayo yakiendelea hivi, familia ya Mbowe imetoa ombi la kumwachia kiongozi huyo ili apate kushiriki maziko ya baba yake mdogo yanayotazamiwa kufanyika siku ya Jumatano, Machame Moshi.
Mbowe alitiwa mbaroni na jeshi la polisi wakati akiwa katika maandalizi ya mwishomwisho kuongoza kongamano la kudai katiba mpya lililopangwa kufanyika jijini Mwanza.
Katika kipindi cha wiki kadhaa chama hicho kimekuwa kikiendesha makongamano ya ndani katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajenda hiyo hiyo moja ya kuamsha vuguvugu la mabadiliko ya katiba.
Suala la katiba mpya ni hoja inayoendelea kutawala vinywani mwa wapinzani wanaodai kuwa katiba ya sasa haitoi uwanja sawa wa ushindani wa kisiasa na chama tawala CCM.