Fatma Karume asema TLS si mali ya umma
23 Aprili 2018Rais wa chama hicho Fatma Karume ambae alichaguliwa hivi karibuni, amewaambia waandishi wa habari kuwa, TLS kuwa chini ya serikali ni kuingilia uhuru wa wanansheria katika kutekeleza majukumu yao hatua ambayo ni kinyume cha sheria na kanuni za kimataifa.
Juma lililopita katika hafla ya kuwaapisha majaji walioteuliwa rais John Magufuli katika hotuba yake alimtaka jaji mkuu nchini profesa Ibahim Juma kuhakikisha anaidhibiti TLS kwa kile alichothibitishiwa kuwa chama hicho ni mali ya umma hivyo lazima kiwe na udhibiti ili kisiwe mali ya mtu binafsi.
Kauli hiyo iliwagutua wanasheria mbalimbali ambao nao ni wananchama wa TLS waliotumia mitandao ya kijamii kupinga vikali kuwa chama hicho hakiwezi kuwa mali ya umma kutokana na tafsiri ya kikatiba juu ya mali ya umma na ukweli kwamba taasisi hiyo imefanya kazi tangu mwaka 1954 ikiwa kama taasisi huru.
TLS inaendeshwa na wanachama wake
Mkataba wa kimataifa wa Harvard ambao Tanzania iliuridhia, unazitaka nchi wanachama kutoingilia uhuru wa wanasheria katika kutekeleza majukumu yao, ambapo katika makubaliano hayo ibara za kumi na sita na ishirini na nne zinazitaka nchi zote kuhakikisha zinawaacha huru wanansheria kufanya kazi zao bila kutishwa wala kudhibitiwa katika kuwahudumia wananchi.
Rais wa TLS Fatma Karume aliechaguliwa Aprili 14 2018 amekanusha vikali kuwa chama hicho si mali ya umma na kusisitiza kwamba haipaswi kuingiliwa wala kudhibitiwa katika kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi, kwani chama hicho kimekuwa kikijiendesha chenyewe kutokana na ada za wananchama wanaolipa kila mwaka na kwa kufanya hivyo ni kuvunja kanuni na sheria za kitaifa na za kimataifa
Kadhalika ameongeza kuwa kitendo cha serikali kudhiti chama hicho katika majukumu yake ni kumnyima haki mwananchi wa kawaida ambae huenda akashtakiwa na serikali ama wale wanaoishtaki serikali kutokana na wanansheria watakaokuwa wanawatetea wananchi kudhibitiwa na serikali.
Hata hivyo baadhi ya wananchi waliozungumza na DW, wamemsihi rais Magufuli aheshimu makubaliano ya kimataifa ambayo watangulizi wake waliyaridhia kwa niaba ya watu wa taifa hilo, na kusisitiza kuwa ni vema mihimili ya nchi ikafanya kazi bila kuingiliana kimajukumu ili taifa liwe na uwajibikaji ulioainishwa katika katiba ya nchi.
Mwandishi:Hawa Bihoga Dw Dar es salaam
Mhariri:Yusuf Saumu