1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yauwa zaidi ya watu 270 Lebanon

Hawa Bihoga
23 Septemba 2024

Mashambulizi ya Israel yamewauwa zaidi ya Walebanon 270 kwenye shambulio baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha takriban mwaka mmoja wa mzozo huo wa Mashariki ya Kati, huku wengine zaidi ya 1,000 wakijeruhiwa.

https://p.dw.com/p/4kzQR
Libanon I Moshi uliotanda baada ya shambulio la Israel.
Mosji mzito ukifuka baada ya shambulio la Israel katika moja ya kijiji kusini mwa Lebanon.Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Jeshi la Israel limetilia mkaazo pia tangazo la kuwataka wakaazi wa kusini na mashariki mwa Lebanon kuyahama makaazi yao kabla ya kampeni ya anga dhidi ya kundi la Hezbollah. 

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon miongoni mwa waliouwawa ama kujeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliofanywa tangu mapema leo ni pamoja na watoto na wahudumu wa afya.

Israel imesema imeyashambulia zaidi ya maeneo mia tatu ambayo yanahusishwa moja kwa moja na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran. Katika mashambulizi hayo zaidi ya watu 1,000 wamejeruhiwa kulingana na mamlaka ya Lebanon.

Maelfu ya raia wamekimbia eneo la kusini kuelekea mji mkuu Beirut katika msafara mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu vita vya Israel na Hezbollah vya mwaka 2006.

Magari yaliojaa wanawake na watoto pamoja na baadhi za samani muhimu yalishuhudiwa kwenye barabara kuu ya kuingia katika mji wa Beirut.

Mmoja wa wanawake aliyekimbia mashambulizi alisema na hapa namnukuu "mashambulizi ni kila upande, milio ni mikubwa, hatuna pakwenda bora kukimbilia katika mji mkuu."

Soma pia:Israel yaanzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon

Baraza la Mawaziri la Lebanon limelazimika kuketi katika mkutano wa dharura kufuatia mzozo huo kuingia hatua mbaya zaidi inayozusha hofu ya kutanuka kwa vita katika eneo la mashariki ya kati.

Nasser Yassin Waziri wa Mazingira Lebanon amesema kwa mipango iliopo ni kuratibu makaazi ya muda kwa wale waliokimbia mashambulizi.

"Ripoti za sasa ni kwamba idadi ya watu waliokimbia makaazi yao wamekimbilia jimbo la Mlima Lebanon na sehemu za Bekaa Magharibi na Beirut." Alisema waziri huyo.

Aliongeza kwamba "kuna mkutano unaendelea sasa hivi wizara ya mambo ya ndani ili kuratibu juhudu za kufungua shule na vituo vya makaazi kwa ajili ya wanaotaka hifadhi."

Kufuatia mkururo huo wa mashambulizi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel inakabiliwa na "siku ngumu" katika wakati ikizidisha mashambulizi yake dhidi ya Hezbollah kusini mwa Lebanon na kurejelea wito wa waziri wake wa Ulinzi wa mshikamano na utulivu wakati jeshi linapotekeleza kampeni hiyo inayoongeza hofu ya kutanuka kwa mzozo huo.

Iran yatuma salamu kwa Israel

Iran inayounga mkono kundi la Hezbollah imeionya Israel kwa kile ilichokiita "matokeo hatari" kufuatia mashambulizi hayo kwenye ngome za Hezbollah nchini Lebanon.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Iran Nasser Kanani aliyafananisha mashambulizi hayo kuwa ya "kiwendawazimu". Kufuatia mzozo huo kuendelea kufukuta Umoja wa Mataifa umeonya kwamba vitendo na matamshi yanaupeleka mzozo wa Mashariki ya Kati "katika hatua nyingine".

Naibu Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon Imrain Riza amesema wanafuatilia kwa ukaribu kile kinachoendelea na kwamba suluhisho la kidiplomasia na kisiasa ndio mwarobaini mwa mzozo huo.

Soma pia:Hofu ya mzozo wa Mashariki ya Kati kusambaa bado yatawala

"Suluhisho wote tunafahamu ni la kisiasa, kidiplomasia na hakika mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa anahimiza sana katika upande huo. Lakini kama tunavyoona siku hadi siku hali ni ngumu kwa raia."

Kundi la Hamas ambalo linapigana na Israel huko Gaza na ni mshirika wa karibu wa Hezbollah limelaani vikali mashambulizi hayo ya Israel na kuyataja kuwa ni ya kinyama na ni sehemu ya uhalifu wa kivita.