1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Hezbollah yaapa kulipa kisasi na "adhabu ya haki" kwa Israel

20 Septemba 2024

Kiongozi wa kundi la Hezbollah amekiri kuwa wanamgambo hao wamepata "pigo” ambalo hawakulitarajia baada ya maelfu ya vifaa vya mawasiliano kulipuka kote nchini Lebanon katika mashambulizi ambayo wameilaumu Israel.

https://p.dw.com/p/4ksTs
Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah
Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan NasrallahPicha: Al Manar TV/AP/picture alliance

Katika hotuba yake ya kwanza tangu mashambulizi hayo kutokea na ambayo yamesababisha vifo vya watu 37 na kuwajeruhi karibu watu 3,000 katika muda wa siku mbili, Nasrallah amesema kamwe hawatoyumbishwa na ameahidi kulipiza kisasi.

Soma pia: Blinken ataka usitishaji vita Gaza ili kukomesha machafuko

Hata wakati alipokuwa anatoa hotuba yake kupitia televisheni, milio ya ndege za kivita za Israel ilisikika mjini Beirut.

Kiongozi huyo wa kundi la Hezbollah ameyaeleza mashambulizi hayo kama "mauaji ya halaiki” na kitendo kinachoweza kutafsiriwa kama vita vya moja kwa moja.

Amesema Israel itakabiliwa na kile alichokiita "kisasi na adhabu ya haki", mahali inapotarajia na pale isipotegemea.