Mashambulizi ya Israel yaendelea kutikisa Gaza
12 Novemba 2023Maafisa wa afya wamesema maelfu ya watoa huduma, wagonjwa na watu wasio na makazi wamenasa kwenye hospitali ya Al-Shifa inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa na ukosefu wa umeme.
Hofu kubwa imetanda miongoni mwa watu hao huku shirika la hisani la madaktari wasio na mipaka likitahadharisha kuwa bila ya usitishwaji wa mapigano au watu kuhamishwa, hospitali ya Al-Shifa itageuka kuwa sehemu ya kuhifadhi maiti.
Soma zaidi: Maelfu ya watu wanasa katika hospitali kubwa ya Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
Ni wakati msaidizi wa waziri wa Afya wa Gaza Youssef Abu Rish akiarifu kuwa mashambulizi ya Israel yameiteketeza wodi ya magonjwa ya moyo ya hospitali hiyo.
Kulingana na Wizara ya afya ya Gaza iliyo chini ya kundi la Hamas, jenereta ya mwisho ya umeme katika hospitali hiyo iliishiwa mafuta Jumamosi na kusababisha vifo vya watoto wawili na wagonjwa wengine wanne. Watoto wengine 37 wako hatarini kufa kutokana na kukosekana kwa umeme.
Hayo yanajiri wakati Israel ikiahidi kuwa itasaidia kuwahamisha watoto kutoka kwenye hospitali hiyo hatua kwa hatua. Licha ya ahadi hiyo, Shirika la afya duniani WHO kupitia mkurugenzi wa kanda, Ahmed al Mandhari limesema jaribio lolote la kuwahamisha wagonjwa kutoka hospitalini hapo itakuwa sawa na kuwahukumu kifo.
Israel yakanusha kushambulia hospitali kwa makusudi
Jeshi la Israel kwa upande wake limekanusha kuwa kwa makusudi, limefanya mashambulizi kuilenga hospitali hiyo ambayo linadai kuwa inatumiwa na Hamas ndani au katika mahandaki yaliyojengwa chini yake. Kundi la Hamas limeyakanusha madai hayo.
Mapema Jumapili jeshi hilo la Israel limetangaza tena kuwapa raia katika eneo la kaskazini lenye mapambano makali muda salama wa saa saba kuondoka kuelekea kusini mwa Palestina. Njia hiyo inayotajwa kuwa salama itakuwa wazi kutokea katika hospitali ya Al-Shifa hadi upande wa kusini mwa Gaza.
Soma zaidi: Netanyahu apuuza miito ya washirika kuwalinda raia wa Gaza
Israel inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka hata kwa washirika wake wa karibu kama Marekani kuhusu mustakabali wa wakazi wa Gaza lakini viongozi wake wameendelea kukataa miito ya kusitisha mapigano. Shirika la kuhudumia wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa UNRWA limnaripoti kuwa hadi sasa watu karibu milioni 1.6 wamekuwa wakimbizi ndani ya Palestina tangu Oktoba 7.
Vita katika Ukanda huo ambavyo vimeshasababisha umwagaji mkubwa wa damu vilianza baada ya wapiganaji wa Hamas kiuivamia Israel Oktoba 7 na kuwauwa watu 1,200. Kulingana na takwimu za sasa za nchi hiyo wapiganaji hao waliwachukua pia mateka 240
Zaidi ya watu 11, 000 wamekufa kutokana na vita Gaza
Matokeo yake, Israeli Ilianzisha mashambulizi ya kulipa kisasi ambayo yamewauwa zaidi ya Wapalestina 11,000 kati yao wakiwemo maelfu ya watoto.Takwimu hizo zilizotolewa na wizara ya afya ya Gaza haijumuishi vifo vilivyotokana na kusitishwa kwa huduma za hospitali.
Hali inaelezwa kuwa mbaya kwenye hospitali ya Al-Shifa ambayo haina maji, umeme, chakula na huduma ya intaneti kwa karibu wagonjwa 600 waliofanyiwa upasuaji, watoto kati ya 37 na 40 pamoja na wagonjwa 17 walio katika vyumba vya wagonjwa mahututi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu limesema kuwa hospitali 20 kati ya 36 za Ukanda wa Gaza hazitoi huduma. Ukanda huo umepokea misaada kiduchu ndani ya wiki tano za vita na Israel imeapa kuendelea kuuzingira hadi pale mateka watakapoachiliwa huru.