Mawaziri wa Mataifa ya G7 wasema Israel ina haki kujilinda
8 Novemba 2023Katika mkutano wao wa siku mbili ulioanza hapo jana, wanadiplomasia hao wamewakosoa wanamgambo wa Hamas na kuiunga mkono Israel wakisema ina haki ya kujilinda, lakini pia wametoa wito wa mapigano kusitishwa kwa muda ili kutoa nafasi ya misaada ya kiutu kufika katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yao ya pamoja mawaziri hao wa mambo ya nje wa kundi la G7, wamekosoa mashambulizi yaliyofanywa na Hamas nchini Israel wakati huo huo wakishinikiza kuchukuliwa hatua za haraka kuwasaidia wapalestina walio na uhitaji mkubwa wa chakula, maji, madawa na makaazi mapya, baada ya wengi wao kupoteza makaazi yao kufuatia mashambulizi yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Soma pia:Mzozo wa Mashariki ya kati wagubika mkutano wa G7 Tokyo
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony Blinken na wenzake kutoka Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan na Italia, wamesisitiza kuwa wanaunga mkono mpango wa kusitisha mapigano kwa muda, kwaajili ya kutoa msaada wa dharura kwa watu wa Gaza na kuachiwa kwa watu wanaoshikiliwa mateka.
Mawaziri hao walikosoa pia vurugu zinazosababishwa na walowezi walio na misimamo mikali dhidi ya wapalestina, wakisema hatua hiyo haikubaliki na inatishia usalama wa ukingo wa Magharibi na pia amani ya kudumu ya kanda hiyo.
Iran yaonywa kuiunga mkono Hamas
Hawakusita pia kuionya Iran dhidi ya kuwaunga mkono wanamgambo wa Hamas na kuchukua hatua zinazoweza kuyumbisha eneo zima la Mashariki ya Kati, ikiwemo pia kuwaunga mkono wanamgambo wa Hezbollah na makundi mengine, na kutumia ushawishi wake kwa makundi hayo kusababisha vurugu za kikanda.
Kingine kilichotiliwa mkazo katika mkutano huo wa siku mbili ulioanza Jana nchini Japan, ni uungaji mkono wa Ukraine katika vita vyake na Urusi.
Kundi hilo limesema usaidizi wake kwa Ukraine hautatetereka huku likiitaka China kutoisaidia Urusi katika mgogoro huo.
Soma pia:Mkutano wa G7 walaani hatua za Korea Kaskazini kuipatia Urusi silaha
Katika taarifa yao ya pamoja wamesema wataendelea kuinga mkono Ukraine katika azma yake ya kupigania uhuru wake.
Ujumbe huo unaokutana mjini Tokyo pia unajadiliana kwa kina kuhusu mipango ya makombora na silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na ongezeko la uchokozi wa China katika mivutano yake ya kikanda na majirani zake.
Fumio Kishida Waziri Mkuu wa Japan amesema umoja wa kundi la G7 unahitajika kwa kiwango kikubwa hasa wakati huu kunakoshuhudiwa migogoro na vita kama vya Mashariki ya kati na Changamoto za eneo la Indo Pacific.
Chanzo: ap/afp