Mawaziri wa mambo ya nje wa G7 wakutana nchini Japan
7 Novemba 2023Mzozo mbaya katika ukanda wa Gaza ambao sasa umedumu kwa muda wa mwezi mmoja pamoja na juhudi za kupunguza athari mbaya za kibinadamu kutokana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel ya shambulio la kundi la Hamas la Oktoba 7, ni masuala ya kipaombele katika mkutano huo. Lakini vita vya Urusi nchini Ukraine, hofu ya Korea kaskazini kwamba huenda inajiandaa kwa majaribio ya nyuklia na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa China duniani, kunaongeza masuala mengine ya mzozo katika agenda ya mkutano huo.
Soma pia: Jeshi la Israel lashambulia maeneo 450 Gaza
Kabla ya kuanza ziara yake ya bara Asia hapo jana, Blinken aliwaamba waandishi wa habari mjini Ankara nchini Uturuki kwamba hata wanapozingatia zaidi mzozo wa Gaza, pia wanajishughulisha sana na kuzingatia kazi muhimu ambayo wanafanya katika kanda ya bahari ya Hindi na Pasifiki na katika sehemu nyingine za dunia.'
Blinken na wenzake kutoka mataifa ya G7 kutafuta msimamo wa üamoja kuhusu mzozo wa Gaza
Mjini Tokyo, Blinken na wenzake kutoka Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan na Italia, watatafuta msimamo wa pamoja kuhusu jinsi ya kushughulikia vita vya Israel na kundi la Hamas ambavyo vinatishia kuyumbisha usalama ambao tayari unatetereka katika eneo kubwa la Mashariki ya Kati na kujaribu kudumisha misimamo iliyopo ya makubaliano kuhusu masuala mengine.
Soma pia: Wapalestina zaidi ya 10 wauwawa kwa shambulio la Israel
Marekani, mshirika muhimu wa Israel, imekataa kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, ikisisitiza kuwa Israel ina haki ya kujibu mashambulizi dhidi yake, ijapokuwa imetoa wito wa kusitishwa kwa muda kwa mapigano hayo kuwezesha kutolewa kwa misaada ya kibinadamu.
Ufaransa ni taifa la pekee la G7 kuunga mkono azimio la baraza kuu la Umoja wa Mataifa
Ufaransa ni mwanachama pekee wa kundi hilo la G7 kupiga kura kuunga mkono azimio la baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita la kutaka kusitishwa mara moja kwa vita hivyo kwa ajili ya kutolewa kwa msaada wa kibinadamu.
Marekani ilipinga azimio hilo huku Japan, Uingereza, Italia, Ujerumani na Canada zikikosa kushiriki katika kura hiyo.
Soma pia: Mashirika ya UN yashinikiza kwa pamoja usitishaji vita Gaza
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock , amesema mkutano huo utajadili jinsi ya kusitishwa kwa mapigano hayo kwa ajili ya kutolewa kwa msaada wa kibinadamu ili kupunguza mateso ya watu katika ukanda wa Gaza.
Viongozi wa Japan na Uingereza wajadili ushirikiano wa kijeshi
Katika hatua nyingine, mawaziri wa mambo ya nje wa Japan na Uingereza, walikutana leo pembezoni mwa mkutano huo wa G7 kujadili ushirikiano wa kina wa kijeshi chini ya makubaliano mapya ya usalama ambayo yanaruhusu wanajeshi wao kuingia katika mataifa hayo mawili kwa mazoezi ya pamoja. Japan na Uingereza zimepanua ushirikiano wao katika miaka ya hivi karibuni huku wasiwasi ukiwa umeongezeka kuhusu ushawishi wa China unaozidi kuimarika.
Soma pia:Marekani, Japan na Korea zaweka makubaliano mapya ya usalama
Japan, ambayo iko katika mkataba wa kijeshi wa pekee na Marekani, imetia saini makubaliano ya ushirikiano huo wa kijeshi na Australia na Uingereza na kuzifanya pia kuwa washirika. Mazungumzo hayo mjini Tokyo kati ya waziri wa mambo ya nje wa Japan Yoko Kamikawa na waziri wa ulinzi Minoru Kihara pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly na waziri wa ulinzi Grant Shapps ni wa kwanza tangu mkataba huo wa ushirikiano wa kijeshi kuanza kutumika katikati ya mwezi Oktoba.