1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mashirika ya UN yashinikiza kwa pamoja usitishaji vita Gaza

6 Novemba 2023

Wakuu wa mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa wametoa wito wa pamoja wa kutaka usitishaji vita mara moja kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4YRym
Moto na moshi waonekana katika anga ya Gaza baada ya mashambulizi ya ndege ya Israel kupiga mji huo Novemba 5, 2023.
Moto na moshi waonekana katika anga ya Gaza baada ya mashambulizi ya ndege ya Israel kupiga mji huo Novemba 5, 2023.Picha: Abed Khaled/AP Photo/picture alliance

Kupitia taarifa ya pamoja, wakuu hao wamerudia wito wao kwa pande husika kwenye vita hivyo kuheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa kuhusu haki za kibinadamu na huduma za kiutu.

Taarifa hiyo imetiwa saini na wakuu wa mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa, miongoni mwao ni shirika linaloratibu misaada ya kiutu OCHA, shirika la mipango ya kimaendeleo la Umoja wa Mataifa, shirika la kuwashughulikia wahamiaji UNHCR na vilevile mashirika ya kimataifa yanayotoa misaada ya Save the Children na Care International miongoni mwa mengine mengi.

Soma pia:UN yahitaji dola bilioni 1.2 kuwasaidia Wapalestina

Taarifa yao ililaani kile walichokiita "mauaji ya kutisha" ya Waisraeli, utekaji nyara uliofanywa na wanamgambo wa Hamas na vilevile makombora yanayofyatuliwa kutoka Gaza.

"Hata hivyo, mauaji zaidi ya kutisha dhidi ya raia katika Gaza, inaghadhabisha, sawa na kuzuia chakula, maji, dawa, umeme na nishati kuwafikia Wapalestina milioni 2.2," taarifa hiyo ilisema.

Soma pia: Netanyahu amuadhibu waziri wake kwa matamshi dhidi ya Gaza

"Siku 30 zimepita. Hii lazima ikome sasa," taarifa ya wakuu hao wa Umoja wa Mataifa ilisisitiza.

Ukanda wa Gaza umezingirwa na Israel, tangu- vita vilipoanza Oktoba 7, wakati wanamgambo wa Hamas walipofanya mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya jamii za Israel.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

Israel 'yaratibu' kwa pamoja na Jordan kudosha misaada muhimu ya matibabu

Baadaye Israel ilianzisha mashambulizi makubwa na makali ya mabomu katika Ukanda wa Gaza, kwa lengo la kuliangamiza kundi la Hamas, ambalo Israel, Marekani na nchi nyingine kadhaa huliorodhesha kuwa la kigaidi.

Katika tukio jingine, jeshi la Israel limesema Jumatatu kupitia taarifa kwamba "iliratibu" kwa pamoja na Jordan kudondosha vifaa muhimu vya matibabu katika hospitali iliyoko uwanjani katika Ukanda wa Gaza.

Mfalme Abdullah II wa Jordan pia alitangaza mapema Jumatatu kwamba jeshi lake la angani lilidondosha msaada muhimu wa kimatibabu katika hospitali hiyo usiku.

Watu 1,400 waliuawa Oktoba 7 wakati wanamgambo wa Hamas waliposhambulia Israel na kuwashika mateka zaidi ya watu 240.

Kulingana na wizara ya Afya inayosimamiwa na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya watu 9,770, theluthi mbili yao ikiwa ni wanawake na watoto.

Israel kuuzingira Ukanda wa Gaza

Vikosi vya Israel vyaugawa Ukanda wa Gaza mara mbili

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa vikosi vya Israel vimeugawa Ukanda wa Gaza katika sehemu mbili, kaskazini na kusini huku mawasiliano katika ukanda huo yakisitishwa mapema Jumattau, hiyo ikiwa ni mara ya tatu tangu vita kuanza.

Soma pia: Jeshi la Israel limetangaza kuuzingira kikamilifu Mji wa Gaza

"Kuzingirwa kwa Mji wa Gaza leo ni hatua kubwa sana katika kuongeza shinikizo la kulisambaratisha kundi la Hamas. Hamas inaelewa maana ya mgawanyiko kati ya kaskazini mwa Ukanda huo na kusini mwa Ukanda huo. Kuhusu swali lako, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, ni njia ya kupitisha misaada ya kibinadamu. Kuna eneo salama zaidi, ni mahali ambapo maji, chakula, na dawa huingia. Mafuta hayataingia," amesema daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel.

Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel
Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la IsraelPicha: Gil Cohen-Magen/AFP

Hayo yamejiri baada ya mashambulizi ya angani ya Israel kushambulia kambi mbili za wahamiaji katika ukanda huo siku ya Jumapili, na kusababisha vifo vya watu kadhaa. Hayo ni kulingana na wizara ya afya ya Gaza.

Juhudi za Antony Blinken kutafuta suluhisho la mzozo wa Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na Rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Amman Jordan Oktoba 17, 2023.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na Rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Amman Jordan Oktoba 17, 2023.Picha: Jacquelyn Martin/POOL/AFP

Tayari Israel imekataa mapendekezo ya Marekani kwamba isitishe vita kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye yuko mashariki ya kati kutafutia mgogoro huo ufumbuzi, amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan mjini Ankara Uturuki. Mwishoni mwa wiki alikutana na rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas na pia Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani.

Aidha mwishoni mwa juma, maelfu ya watu waliendelea kujitokeza katika mitaa ya miji mbalimbali ikiwemo Washington, Paris, na Dusseldorf kutetea Wapalestina na kutaka vita visitishwe.

Vyanzo: DPAE, APE, AFPE