1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu apuuza miito ya washirika kuwalinda raia wa Gaza

11 Novemba 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepuuza miito ya washirika wake wa mataifa ya magharibi iliyoihimiza nchi hiyo kufanya kazi ya ziada kuwalinda raia kwenye kampeni yake ya kijeshi huko Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4YhSn
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Xinhua/IMAGO

Miito hiyo imefuatia ongezeko la idadi ya vifo vya raia wa Kipalestina kutokana na hujuma nzito za jeshi la Israel linalopambana kundi la Hamas ambalo lilifanya shambulizi kubwa lililowauwa watu 1,200 ndani ya ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7.

Waziri Mkuu Netanyahu amesema kundi la Hamas ndiyo linabeba dhima ya athari zozote zinazowakumba wakaazi wa Ukanda wa Gaza akirejea madai yake kwamba kundi hilo linawatumia raia kama ngao kwenye operesheni zake.

Mamtashi hayo ameyatoa baada ya rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kutoa mwito wa kusitishwa mapigano huku waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken akiitaka Israel ijiepushe na mashambulizi yanayowauwa raia.