1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Uingereza zashambulia maeneo ya Kihouthi

Sylvia Mwehozi
12 Januari 2024

Rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa vikosi vya kijeshi vya nchi yake na Uingereza vimefanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo kadhaa nchini Yemen yanayotumiwa na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

https://p.dw.com/p/4b9OT
Shambulizi la angani
Shambulizi la anga kuelekea maeneo ya waasi wa KihouthiPicha: Royal Air Force/dpa/picture alliance

Hatua hiyo inafuatia mashambulizi ya waasi hao ambayo wameyafanya dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu.

Mashambulizi hayo ya angani yamepiga miji kadhaa ya Yemen, ambako waasi wa Kihouthi wanadhibiti maeneo mengi na kuhusisha ndege za kivita na makombora ya Tomohawk, kwa mujibu wa vyombo tofauti vya Marekani.

Katika taarifa yake, Biden ameyataja mashambulizi hayo kuwa ni "jibu la moja kwa moja" kwa mashambulizi "yasiyokuwa ya kawaida" ya Wahouthi, "ikiwa ni pamoja na matumizi ya makombora ya Balistiki ya kuzuia meli kwa mara ya kwanza katika historia."

"Leo, kwa maelekezo yangu, vikosi vya kijeshi vya Marekani pamoja na Uingereza na kwa usaidizi kutoka Australia, Bahrain, Canada na Uholanzi, vilifanikiwa kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo kadhaa nchini Yemen yanayotumiwa na waasi wa Kihouthi kuhatarisha uhuru na usafirishaji katika mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini duniani", alisema Biden.

Yemen
Afisa wa usalama wa waasi wa KihouthiPicha: Osamah Yahya/Zuma/picture alliance

Mkakati wa Marekani: Marekani yazima shambulizi ya Wahouthi huko Bahari ya Shamu

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak pia aliitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri mjini London siku ya Alhamisi kujadili mashambulizi dhidi ya Wahouthi.

Marekani na washirika wake walikuwa wametoa onyo kali zaidi kwa Wahouthi kusitisha mashambulizi ya meli, ingawa Washington imekuwa makini kuhusu hatari ya kuzidisha mivutano ya kikanda.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano lilipitisha azimio la kusitishwa mara mojakwa mashambulizi ya meli za kibiashara, na kuonya kuwa ni kitisho kwa amani na usalama wa kikanda.

Kuongezeka kwa mashambulizi hayo kumesababisha makampuni ya meli kukwepa njia hiyo na badala yake kugeukia Cape of Good Hope nchini Afrika Kusini, na hivyo kuzua hofu ya mkwamo mwingine wa uchumi wa dunia. Wahouthi wanasema wanalenga tu meli zinazohusishwa na Israel au washirika wake.

Waasi wa Kihouthi
Wapiganaji wa kihouthi wakitembea kwenye meli katika Bahari ya Shamu katika picha iliyotolewa Novemba 20, 2023Picha: Houthi Military Media/REUTERS

Mashambulizi hayo yanahatarisha kugeuza hali ambayo tayari ni ya wasiwasi katika kanda ya Mashariki ya Kati kuwa mzozo mpana unaozishindanisha Marekani na Israel dhidi ya Iran na washirika wake wa kikanda.

soma taarifa hii: Bahari ya Sham: Kwanini mataifa ya Kiarabu hayajajiunga na muungano wa vikosi vya wanamaji

Kiongozi wa kundi hilo la waasi Abdul-Malik al-Houthi ameapa kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi hayo ya anga ya kimataifa. Ameonya kwamba "uchokozi wowote wa Marekani hautopita bila kushughulikiwa".

Waasi wa Kihouthi wamefanya mashambulizi kadhaa katika njia muhimu ya kimataifa ya baharini tangu kuzuka kwa vita vya Gaza na shambulizi la kushutukiza la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7.