1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Mataifa ya Kiarabu yakataa kujiunga na muungano wa wanamaji

Cathrin Schaer Bakari Ubena
28 Desemba 2023

Wakati Marekani ilipotangaza wiki iliyopita kuanzisha muungano wa vikosi vya wanamaji ili kulinda meli za kibiashara zinazosafiri katika Bahari Nyekundu, walieleza kwamba karibu nchi 10 zingelishiriki katika hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/4afHd
Wapiganaji wa kundi la Houthi
Wapiganaji wa kundi la HouthiPicha: Osamah Yahya/Zuma/IMAGO

Maswali yameibuka mara baada ya baadhi ya mataifa makubwa ya Kiarabu kutojiunga na muungano huo. 

Tangu katikati mwa mwezi Novemba, kundi la waasi wa Houthi nchini Yemen limekuwa likifyatua maroketi na kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwa kuzilenga meli zinazosafiri kupitia Mlango wa bahari wa Bab el-Mandeb.

Afisa mwandamizi wa Houthi alieleza kwenye mitandao ya kijamii kwamba vitendo hivyo vitaendelea "hadi uhalifu wa mauaji ya kimbari huko Gaza ukomeshwe na pia chakula, dawa na mafuta viruhusiwe kuingia katika eneo hilo ambalo raia wake wamezingirwa."

Soma pia: Marekani yazima shambulizi ya Wahouthi huko Bahari ya Shamu

Mtaalam wa eneo la Mashariki ya Kati Daniel Gerlach anasema waasi wa Houthi wanatumia uadui wao na Israel kwa malengo yao ya kimkakati. "Uadui na Israel ni hatua ya kimkakati kwa Wahouthi, na pia ni sehemu ya madai yao kwamba Israel ni adui yao mkuu ingawa kwa kweli hakuna mzozo wa moja kwa moja na Israel. Lakini wanataka kuonyesha ulimwengu wa waislamu na mataifa ya Kiarabu kwamba wako upande wa Wapalestina."

Mnamo Novemba 19, waasi wa Houthi wamekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Yemen tangu mwaka 2015 na ambao sasa wanadhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo, waliiteka meli ya mizigo ya Galaxy Leader inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Israel.

 

Meli nyingine zimeshambuliwa na ndege zisizo na rubani

Helikopta ya kijeshi ya Houthi baada ya wapiganaji wake kuivamia meli ya mizigo ya Galaxy Leader
Helikopta ya kijeshi ya Houthi baada ya wapiganaji wake kuivamia meli ya mizigo ya Galaxy LeaderPicha: Houthi Military Media/REUTERS

Matukio hayo yalishuhudiwa zaidi katika mlango wa bahari wa Bab el-Mandeb wenye upana wa karibu kilomita 32  na unaounganisha Ghuba ya Aden na Bahari Nyekundu.

Meli nyingi hupitia eneo hilo ili kuufikia Mfereji wa Suez lakini pia ni njia fupi zaidi inayounganisha bara la Ulaya na Asia. Matokeo yake, makampuni makubwa ya usafirishaji baharini yameepuka kupita kwenye mlango huo wa bahari.

Muungano wa vikosi vya wanamaji uliopendekezwa na kuongozwa na Marekani ili kulinda meli za kibiashara dhidi ya vitisho vya waasi wa Houthi ulipewa jina la "Operation Prosperity Guardian" na Marekani iliwaomba kujiunga wanachama wengine 38 wa kile kinachojulikana kama "Combined Maritime Forces", yaani muungano wa usalama wa baharini unaoongozwa na Marekani katika Mashariki ya Kati.

Soma pia: Wahouthi wazishambulia meli za Marekani kwa droni

Kufikia sasa ni nchi 10 tu ambazo zimesema hadharani zitajiunga na muungano huo. Nazo ni Bahrain, Canada, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Norway, Uhispania, Ushelisheli na Uingereza. Lakini baadaye, maswali kadhaa yaliibuka.

Serikali ya Uhispania ilikanusha kujiunga kwake, Ufaransa ilionyesha wasiwasi kwamba ushiriki wao katika muungano huo ungeweza kuvuruga shughuli zao zingine huku Italia ikisisitiza kuwa meli zao zitabaki chini ya mamlaka ya taifa hilo.

Lakini swali kuu lilikuwa ni kutojiunga kwa mataifa makubwa zaidi ya Mashariki ya Kati isipokuwa Bahrain ambayo inazihifadhi meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani. Wataalam wanasema Misri imehofia kujiunga ili kutozusha mvutano utakaopelekea kufungwa kwa Mfereji wa suez ambao ni mali yake na chanzo kikubwa cha mapato cha hadi dola milioni 10 kwa mwaka.

Saudi Arabia nayo imeshindwa kujiunga ili kuhofia kuvuruga harakati zake za mazungumzo ya amani na WaHouthi wa Yemen lakini pia nia ya kurekebisha mahusiano na wafadhili wao Iran.

Licha ya kuwa na msimamo mkali dhidi ya Wahouthi Umoja wa Falme za Kiarabu haukujiunga na muungano huo.

Wachambuzi wanasema kuwa mataifa hayo matatu yenye ushawishi mkubwa katika Bahari Nyeusi hayataki kuchukua hatua itakayotafsiriwa kwamba wanadhamiria kuilinda Israel.